HAMAS: Kuwatia mbaroni Wapalestina kutashamirisha Intifadha
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i8998-hamas_kuwatia_mbaroni_wapalestina_kutashamirisha_intifadha
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesistiza kuwa kitendo cha askari wa utawala wa Kizayuni cha kuwatia nguvuni Wapalestina kitashamirisha na kupanua zaidi Intifadha ya Quds.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2016 11:00 UTC
  • HAMAS: Kuwatia mbaroni Wapalestina kutashamirisha Intifadha

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesistiza kuwa kitendo cha askari wa utawala wa Kizayuni cha kuwatia nguvuni Wapalestina kitashamirisha na kupanua zaidi Intifadha ya Quds.

Katika taarifa yake, HAMAS imelaani wimbi kubwa la kamatakamata na utiaji nguvuni Wapalestina katika eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na kusisitiza kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel hautoweza katu kufikia malengo na matakwa yake kwa kuwatia nguvuni Wapalestina.

Taarifa ya Hamas imefafanua kuwa kuwatia nguvuni Wapalestina kutawafanya wawe na azma thabiti zaidi ya kuendeleza mapambano yao.

HAMAS imeongeza kuwa jinai za adui wa Kizayuni na hatua za Mamlaka ya Ndani ya Palestina zinazolenga kuidhibiti na kuzima Intifadha na ushirikiano wa kiusalama wa Mamlaka hiyo na maghasibu wa Kizayuni havitoweza katu kusimamisha mapambano na muqawama wa wananchi wa Palestina wa kukabiliana na wavamizi wa Kizayuni.

Asasi ya kushughulikia Wapalestina waliofungwa na walioachiwa huru kutoka jela za utawala wa Kizayuni imetangaza hivi karibuni kuwa kushtadi wimbi la kamatakamata na utiaji nguvuni Wapalestina kumeufanya utawala wa Kizayuni uanzishe makumi ya jela mpya na mahabusu ambazo zina hali mbaya zaidi kuliko jela za huko nyuma.

Hivi sasa kuna Wapalestina wapatao elfu saba katika magereza na mahabusu yapatayo 22 ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Miongoni mwa Wapalestina hao ni watoto mia nne na wanawake sabini.../