Imran Khan: Maandamano ya kupinga serikali kuendelea tena kesho
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i90226-imran_khan_maandamano_ya_kupinga_serikali_kuendelea_tena_kesho
Imran Khan Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan amesema kuwa, maandamano ya kuipinga serikali kuelekea mji mkuu Islamabad yataendelea tena kesho Jumanne.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 07, 2022 09:13 UTC
  • Imran Khan: Maandamano ya kupinga serikali kuendelea tena kesho

Imran Khan Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan amesema kuwa, maandamano ya kuipinga serikali kuelekea mji mkuu Islamabad yataendelea tena kesho Jumanne.

Maandamano hayo yalisitishwa katika wilaya ya Wazirabad mashariki mwa mkoa wa Punjab baada ya Imran Khan kujeruhiwa kwa risasi siku ya Alkhamisi katika jaribio la kutaka kumuua.

Mfuasi mmoja wa Imran Khan aliuliwa na wengine 13 walijeruhiwa katika hujuma hiyo. Akizungumza akiwa kwenye kiti cha magurudumu katika hospitali ya Shaukat Khanun alikokuwa amelazwa, Imran Khan amerudia tena matakwa yake kutaka uchunguzi ufanywe kuhusu kushambuliwa kwa risasi na anataka maafisa watatu wenye mamlaka makubwa serikalini na jeshini wajiuzulu akidai walihusika kupanga shambulizi dhidi yake. Imran Khan jana aliruhusiwa kutoka hospitali. Serikali ya waziri mkuu Shehbaz Sharif imekanusha kuhusika kwa namna yoyote, na badala yake imesema jaribio la kumuua Imran Khan lilifanywa na mtu aliyebeba bunduki aliyochochewa na "itikadi kali za kidini".

Imran Khan baada ya kujeruhiwa katika shambulio la risasi

 

Takriban miezi sita iliyopita, Imran Khan aliondolewa kwenye wadhifa wa uwaziri mkuu wa Pakistan baada ya wabunge kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye. Imran Khan, ambaye anataka ufanyike uchaguzi wa mapema, bila shaka atashikilia zaidi takwa lake hilo kutokana na ushindi huo aliopata.

Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa kriketi mwenye umri wa miaka 70 amekuwa akiongoza msafara wa maelfu ya watu, wa kampeni iliyoanza wiki iliyopita ya kuandamana kutoka Lahore hadi Islamabad. Imran Khan amewataka wafuasi wake kuendelea na maandamano hayo kuelekea mji mkuu huo wa Pakistan.