Al Azhar yalaani jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina
Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar nchini Misri kwa mara nyingine tena kimeutaka ulimwengu uzingatie machungu na mateso ya taifa la Palestina na kukaliwa kwa mabavu ardhi sambamba na kulaani jinai za umwagaji damu zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi Wapalestina.
Al-Azhar imetoa taarifa hiyo kali dhidi ya Uzayuni kwa mnasaba wa kumbukumbu mbaya zaidi ya historia ya kisasa ambayo ni kumbukumbu ya kugawanywa Palestina, na ambayo inasadifiana na Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Taifa la Palestina, ambayo ni Novemba 29 kila mwaka.
Kwa mujibu wa tovuti ya "Rai Al Youm", kwa mnasaba huu, Al-Azhar kwa mara nyingine tena imesisitiza azma yake ya kudumu ya kuliunga mkono taifa la Palestina na mapambano yake ya kisheria na halali ya ukombozi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel. Aidha Al Azhar imetangaza upinzani wake kamili dhidi ya njama zote za Wazayuni za uyahudishaji ambazo zinafanyika kwa lengo la kutaka kubadilisha utambulisho, na muundo wa idadi ya watu wa Palestina na kunyakua ardhi zao zote.
Katika taarifa hiyo, Al-Azhar imesisitiza kwamba vitendo hivyo vya Wazayuni vinaonyesha utambulisho halisi wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ni utamblisho wa umwagaji damu na ukatili.
Katika taarifa hiyo inasisitizwa kuwa, mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kamwe hayatasahau ukatili, mauaji ya halaiki na jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya taifa la Palestina.
Al Azhar imesema uhalifu huo hauwezi kufutika katika kumbukumbu za ubinadamu hata kama utawala wa Kizayuni unajaribu kupotosha historia.
Al-Azhar inaiomba jumuiya ya kimataifa kusimama pamoja na taifa la Palestina na kuunga mkono mapambano yake halali dhidi ya utawala dhalimu wa Kizayuni na vitendo vyake vya kigaidi.
Ikumbukwe kuwa, mwaka 1977 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza tarehe 29 Novemba kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Taifa la Palestina. Sababu ya hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa ni nafasi na mchango wa Baraza Kuu la umoja huo katika kuigawa ardhi ya Palestina.