Wamorocco washerehekea ushindi Kombe la Dunia kwa kuiunga mkono Palestina
Dec 02, 2022 04:25 UTC
Mashabiki wa timu ya taifa ya soka ya Morocco wamesikika wakipiga nara na kaulimbiu za kuiunga mkono Palestina baada ya timu yao kufuzu kuingia hatua ya mtoano ya fainali za Kombe la Dunia la 2022 zinazofanyika nchini Qatar.
Katika michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka huu, Waislamu katika sehemu mbalimbali za mikusanyiko nchini Qatar wamekuwa mara nyingi wakipeperusha bendera ya Palestina kuwaunga mkono wananchi wa taifa hilo linaloendelea kudhulumiwa kwa zaidi ya miaka 70 sasa na kuonyesha chuki zao kwa jinai wanazofanyiwa Wapalestina na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Tovuti ya televisheni ya Al-Alam imeonyesha picha na video za mashabiki wa timu ya taifa ya soka ya Morocco wanaoonekana wakitoa nara na kaulimbiu za kuunga mkono Palestina baada ya timu ya taifa ya soka ya Morocco kutinga hatua ya mtoano ya michuano ya Kombe la Dunia la 2022 inayoendelea nchini Qatar.
Mbali na kutangaza uungaji mkono wao kwa Wapalestina, watazamaji wa mashindano ya soka ya Kombe la Dunia la 2022 Qatar hususan kutoka mataifa ya Kiarabu wameyatumia mashindano hayo kudhihirisha pia chuki zao dhidi ya Israel kwa kukataa kuhojiwa na waandishi wa habari kutoka utawala huo dhalimu wa Kizayuni.
Katika mechi ya raundi ya tatu ya hatua ya makundi katika kundi F, timu za Morocco na Kanada zilipambana hapo jana, ambapo mechi hiyo ilimalizika ushindi wa Morocco wa mabao mawili kwa moja.
Ushindi huo umeiwezesha timu ya taifa ya nchi hiyo kuongoza kundi hilo ikifuatiwa na Croatia.../