Haniya: Wapalestina watashadidisha mapambano dhidi ya ujenzi haramu wa Israel
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ameionya Israel dhidi ya sera yake ya unyakuzi wa ardhi na kusisitiza kuwa, ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni utakabiliwa kwa nguvu kupitia muqawama.
Ismail Haniya amesema hayo leo Alkhamisi akijibu matamshi yaliyotolewa na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu ajaye wa utawala wa Kizayuni aliyedai kuwa, ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina ndicho kipaumbele kikuu cha serikali yake.
Haniya amesema sera na misimamo ya kisiasa ya serikali ya Netanyahu itazidi kuvuruga hali ya mambo katika eneo na kueleza bayana kwamba, kipaumbele cha Wapalestina ni kukabiliana na sera hizo za utawala mpya wa Kizayuni kupitia muqawama na umoja.
Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina ameongeza kuwa, Wapalestina katu hawatouruhusu utawala haramu wa Israel utekeleza njama na mipango yake michafu dhidi ya maeneo yake hususan mji mtakatifu wa Quds na Masjidul Aqsa.
Jana Jumatano, Netanyahu alisema ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ndicho kipaumbele kikuu cha baraza lake la mawaziri.
Alisema ujenzi huo haramu katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu utafanyika kwa nguvu zaidi katika eneo la Galilee, Jangwa la Negev, Miinuko ya Golan, na vilevile maeneo ya Judea na Samaria katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.