Biashara ya bidhaa za Iran yazidi kunawiri nchini Saudi Arabia
(last modified Tue, 10 Jan 2023 02:29:29 GMT )
Jan 10, 2023 02:29 UTC
  • Biashara ya bidhaa za Iran yazidi kunawiri nchini Saudi Arabia

Usafirishaji nje wa bidhaa za Iran kuelekea nchini Saudi Arabia umestawi hivi sasa baada ya kuanza mazungumzo baina ya nchi hizi mbili za Waislamu. Hayo yametokea baada ya biashara baina ya pande mbili kuzorota kwa miaka kadhaa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Sayyid Rohollahi Latifi, mjumbe wa Kamati ya Kimataifa na Biashara za Nje ya Wizara ya Viwanda, Madini na Biashara ya Iran ametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa Kiirani wa 1401 Hijria Shamsia yaani mwisho ma mwezi Machi 2022, zaidi ya tani 30,791 za bidhaa za Iran zenye thamani ya dola milioni 14 na laki saba na 10,331 zimesafirishwa hadi Saudi Arabia na hilo ni ongezeko kubwa la bidhaa za Iran kuelekea Saudia kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Amesema, mwaka jana, bidhaa za Iran zilizopelekwa Saudi Arabia zilikuwa na thamani ya chini ya dola 42,000.

Iran ni mzalishaji mkubwa wa bidhaa za kila aina katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Asia Magharibi

 

Mwaka 2016, Saudia ilikata uhusiano wake wa kidiplomasia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kisingizio cha kushambuliwa ubalozi wake wa Tehran na ubalozi wake mdogo wa mjini Mash'had, kaskazini mashariki kwa Iran. Lakini mazungumzo yanaendelea baina ya pande mbili na hadi hivi sasa kumeshafanyika awamu tano za mazungumzo baina ya Iran na Saudia huko Baghdad, mji mkuu wa Iraq.

Mjumbe wa Kamati ya Kimataifa na Biashara za Nje ya Wizara ya Viwanda, Madini na Biashara ya Iran pia amesema, kadiri mazungumzo baina ya Tehran na Riyadh yanavyozidi kuwa mazuri kwa upatanishi wa Iraq, uhusiano wa pande mbili hasa wa kibiashara baina ya nchi mbili nao unazidi kustawi.

Tags