HAMAS: Tuna matumaini ya kivuko cha Rafah kufunguliwa moja kwa moja
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i9337-hamas_tuna_matumaini_ya_kivuko_cha_rafah_kufunguliwa_moja_kwa_moja
Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema wana matumaini ya kufunguliwa moja kwa moja kivuko cha Rafah ambacho ni kivuko muhimu zaidi kinachounganisha eneo la Ukanda wa Gaza, Palestina na ulimwengu wa nje.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 17, 2016 00:12 UTC
  • HAMAS: Tuna matumaini ya kivuko cha Rafah kufunguliwa moja kwa moja

Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema wana matumaini ya kufunguliwa moja kwa moja kivuko cha Rafah ambacho ni kivuko muhimu zaidi kinachounganisha eneo la Ukanda wa Gaza, Palestina na ulimwengu wa nje.

Mahmoud al-Zahar ameeleza kuwa harakati hiyo inakaribia kufikia makubaliano na Shirika la Usalama na Intelijinsia la Misri kuhusu utaratibu mpya wa ufanyaji kazi kivuko cha Rafah katika mpaka wa pamoja wa Gaza na Misri na wana matumaini kuwa utaratibu utakaotumika utawezesha kivuko hicho kuendelea kuwa wazi moja kwa moja.

Kwa mujibu wa Dakta al-Zahar, suala muhimu zaidi lililojadiliwa katika mazungumzo baina ya ujumbe wa Hamas na maafisa wa usalama na intelijinsia wa Misri ni suala la usalama na kuongeza kuwa, kwa masikitiko, vyombo vingi vya habari vya Misri huko nyuma vilikuwa vikieneza habari zisizo sahihi za kuihusisha harakati ya Hamas na matukio ya kiusalama ya nchi hiyo, lakini katika mazungumzo ya karibuni, harakati hiyo imetoa majibu kwa tuhuma zote hizo.

Kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas amesema, Hamas haiingilii masuala ya ndani ya Misri wala haiungi mkono upande wowote unaotaka kuhujumu usalama wa taifa wa Misri au wa nchi nyengine yoyote ya Kiarabu.

Ujumbe wa Hamas unatazamiwa kuelekea Misri mnamo siku zijazo kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo yake na maafisa wa usalama wa nchi hiyo.

Hatua ya serikali ya Misri ya kukifunga kivuko cha Rafah ambayo ndiyo njia pekee ya kuingilia na kutokea wakaazi wa Gaza imesababisha masaibu na matatizo makubwa ya kibinadamu na kiuchumi kwa Wapalestina wapatao milioni moja na laki tisa wanaoishi katika eneo hilo lililowekewa mzingiro kwa takriban miaka 10 sasa na utawala wa Kizayuni wa Israel.../