Ujumbe wa Muungano wa Mabunge ya Kiarabu wawasili Damascus, Syria
Muungano wa Mabunge ya Kiarabu sambamba na kuunga mkono kurejeshewa nafasi yake Syria iliyokuwa nayo katika mataifa ya Kiarabu imesema kuwa, ujumbe wa muungano huo umeelekea nchini Syria.
Uamuzi wa kutuma ujumbe wa muungano huo ulifikiwa katika mkutano wa 34 wa Muungano wa Mabunge ya Kiarabu uliofanyika jana katika mji mkuu wa Iraq Baghdad.
Taarifa ya mwisho ya mkutano huo ilisisitiza kuwa, kuna haja ya kuhuishwa uhusiano wa Syria na mataifa ya Kiarabu na kurejea kama ulivyokuwa hapo kabla.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kwamba, kuna haja kwa diplomasia ya Kibunge baina ya mataifa ya Kiarabu kuwa amilifu ili kuweko diplomasia rasmi baina ya mataifa ya Kiarabu na nchi ya Syria.
Kadhalika taarifa hiyo imesisitiza kuungwa mkono kadhia ya Palestina na kueleza bayana kwamba, hilo ndilo suala kuu baina ya mataifa ya Kiarabu na Waislamu.
Kabla ya hapo Mohamed al-Halbousi, Spika wa Bunge la Iraq akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Muungano wa Mabunge ya Kiarabu alieleza kwamba: Tunazitaka nchi za Kiarabu zichukue maamuzi ya kuirejesha nchi ya Syriia katika nafasi yake miongoni mwa mataifa ya Kiarabu.
Mnamo mwaka 2011 na kwa mashinikizo ya Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) na Saudi Arabia kufuatia kuanza kwa mgogoro nchini Syria, Arab League ilichukua hatua ya kusimamisha uwanachama wa nchi hiyo ya Kiarabu katika jumuiya hiyo, huku nchi nyingi za Kiarabu zikiamua kufunga balozi zao na kuvunja uhusiano wao wa kidiplomasia na serikali ya Damascus.