Ben Gvir atoa amri ya Wazayuni wenzake kupigwa risasi
Itamar Ben Gvir, kiongozi wa chama cha Mayahudi wenye misimamo mikali ambaye pia ni Waziri wa Usalama wa Ndani katika baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu, tangu apewe nafasi hiyo amekuwa akiwapa silaha walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuwachochea wawaue kiholela Wapalestina wasio na hatia.
Baada ya wiki 8 za maandamano ya amani yanayofanywa na wapinzani wa Netanyahu, hatimaye ametoa amri ya kupigwa risasi waandamanaji ikiwa ni katika kile kinachotathminiwa kuwa ni marekebisho ya sheria ya mfumo wa mahakama za utawala haramu wa Israel, ambapo tayari wapinzani 11 wa Netanyahu wamepigwa risasi na kujeruhiwa huku wengine zaidi ya 30 wakikamatwa.
Ili kuwashawishi polisi watii amri zake, Ben Gvir hivi karibuni ameongeza mishahara ya polisi na kwa kuzingatia kuwa Wizara ya Fedha ya utawala huo imekabidhiwa Bezalel Yoel Smotrich, kiongozi mwingine wa chama cha Kizayuni chenye misimamo mikali ya kidini, hivyo Ben Gvir hana tatizo katika kudhamni pesa zinazohitajika kwa ajili ya kusukuma mbele mipango yake.
Baada ya polisi kuamua kutumia mabavu na vurugu dhidi ya wapinzani wa Netanyahu, kuna uwezekano mkubwa kwamba wapinzani na waandamanaji nao pia watatumia mabavu na silaha katika kukabiliana na polisi. Suala hilo linaonekana kupata nguvu zaidi ikitiliwa maanani kuwa siku chache zilizopita, wapinzani wa Netanyahu waliiba kifaru kimoja kutoka kwenye kambi ya jeshi na kukitumia katika maandamano yao na hivyo kutuma ujumbe wa moja kwa moja kwa serikali kwamba maandamano yao hayatakomea katika harakati za kiraia pekee.
Kwa kuzingatia kuwa jeshi pia liko upande wa wapinzani, hivyo kuna uwezekano wa wapinzani na waandamanaji kupewa silaha na jeshi hilo. Ikiwa Wizara ya Usalama wa Ndani chini ya uongozi wa Itamar Ben Gvir itaimarisha na kuwapa silaha polisi na waungaji mkono wa serikali ya Netanyahu, jeshi pia lina uwezo wa kuwapa silaha na zana za kivita wapinzani, ambapo jambo hilo linaweza kuongeza utata na upeo wa migogoro na hitilafu za ndani katika utawala huo wa kibaguzi.
Jambo lingine muhimu katika uwanja huo ni kwamba chanzo cha mzozo uliopo kati ya pande mbili zinazozozana, yaani sheria ya marekebisho ya mfumo wa mahakama, ni suala ambalo halitoa uwezekano wowote wa kufikiwa muwafaka kati ya pande hizo na wote wanalichukulia kuwa ima wapate ushindi au kushindwa. Kwa ibara nyingine ni kuwa ni kadhia ya uhai na kifo.
Netanyahu anaitazama sheria ya mageuzi ya mahakama kama malaika wake mwokozi ili kuepuka kesi zinazomkabili mahakamani na iwapo itapitishwa, anataka kuitumia katika juhudi zake za kuondoa vyombo vya mahakama na hasa Mahakama ya Juu katika mikono ya wapinzani na hivyo kuilemaza kabisa. Kwa kufanya hivyo anataka kujibunia kinga ya kimahakama mbele ya wapinzani. Katika upande wa pili wapinzani wanasema kuwa iwapo sheria hiyo ya mageuzi ya mahakama itapitishwa, Israeli italazimika kuaga kwaheri milele kile kinachodaiwa kuwa ni 'nembo ya demokrasia' katika eneo. Kwa kuzingatia kuimarishwa nafasi ya kijamii ya vyama vya mrengo wa kulia, vyama vya kisekulari havitakuwa tena na nafasi ya kisiasa katika jamii ya Wazayuni huko Israel na hivyo wafuasi wake watalazimika kuhama na kwenda kuishi katika nchi nyingine za dunia.
Kwa hiyo, moja ya matokeo ya mpango wa mageuzi ya mahakama itakuwa ni kuongeza kasi ya uhamiaji wa kinyume nyume na kuondolewa uwekezaji huko Israeli. Hii ni pamoja na ukweli kwamba migogoro ya ndani imeongezeka katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na kuna wasiwasi juu ya kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe katika utawala huo. Pia kuna uwezekano kwamba serikali ya sasa ya Israeli itakabiliwa na hatima ile ile ya serikali zilizopita za Mayahudi huko nyuma ambapo Israeli inatazamiwa kutofikia maadhimisho ya miaka 80 ya kuasisiwa kwake.