Ansarullah: Mazungumzo yakivunjika tutaingia kwenye vita vya kuamua hatima ya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i94894-ansarullah_mazungumzo_yakivunjika_tutaingia_kwenye_vita_vya_kuamua_hatima_ya_yemen
Mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema iwapo mazungumzo ya hivi sasa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia yatafeli, vita vikali vitaanza vya kuhitimisha uchokozi na uvamizi huo.
(last modified 2026-07-31T06:29:55+00:00 )
Mar 09, 2023 03:11 UTC
  • Ansarullah: Mazungumzo yakivunjika tutaingia kwenye vita vya kuamua hatima ya Yemen

Mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema iwapo mazungumzo ya hivi sasa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia yatafeli, vita vikali vitaanza vya kuhitimisha uchokozi na uvamizi huo.

Kituo cha habari cha Al-Mayadeen kimeripoti leo kuwa Muhammad Al-Bukhaiti, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba, mazungumzo hayo huenda yasifaulu na hivyo nchi hiyo kulazimika kuingia katika vita vya kuamua hatima yake kwa kukomesha uvamizi na kuondoa mzingiro iliowekewa.
Katika ujumbe wake huo wa Twitter, Al-Bukhaiti amewaasa Wayemeni ambao bado wako pamoja na muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia wajiunge na safu za Ansarullah ili waweze kukamilisha hatima ya vita hivyo haraka iwezekanavyo.
Halikadhalika, mjumbe huyo wa ofisi ya kisiasa ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema, kuwepo Marekani nchini Yemen ni mwendelezo wa operesheni za muungano wa Saudia na kwamba ukweli halisi kuhusiana na uchokozi wa muungano huo dhidi ya nchi hiyo umewadhihirikia watu wote.
Hujuma za kijeshi za Saudia na waitifaki wake Yemen

Kabla ya hapo, Al-Bukhaiti aliwahi kusema kwamba, Marekani na Uingereza hazitaki suluhu na amani ipatikane Yemen na kwamba kila wanapohisi kuna maendeleo yamepatikana katika mazungumzo hayo, hujaribu kufanya kila njia ili hatua zilizopigwa zisiwe na tija; hivyo amesisitiza kuwa, endapo mazungumzo hayatafanikiwa chaguo la hatua za kijeshi za kila upande litabaki kuwepo mezani.

Kwa uungaji mkono wa Marekani, Muungano wa Falme za Kiarabu na nchi nyingine kadhaa, Saudi Arabia ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen tangu Machi 2015 na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, baharini na angani. Moto wa vita uliowashwa na Saudi Arabia na waitifaki wake huko Yemen umesababisha vifo na kujeruhiwa mamia ya maelfu ya Wayemen, mbali na wengine milioni nne waliogeuka wakimbizi baada ya kulazimika kuyahama makazi yao.../