UNICEF: Mamilioni ya watoto wanakabiliwa na hatari ya utapiamlo nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i95482-unicef_mamilioni_ya_watoto_wanakabiliwa_na_hatari_ya_utapiamlo_nchini_yemen
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umeonya kuwa mamilioni ya watoto wanakabiliwa na hatari ya utapiamlo nchini Yemen ikiwa fedha hazitatolewa haraka kwa nchi hiyo ya Kiarabu iliyokumbwa na vita, ambapo mtoto mmoja hufariki dunia kila baada ya dakika kumi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 24, 2023 22:50 UTC
  • UNICEF: Mamilioni ya watoto wanakabiliwa na hatari ya utapiamlo nchini Yemen

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umeonya kuwa mamilioni ya watoto wanakabiliwa na hatari ya utapiamlo nchini Yemen ikiwa fedha hazitatolewa haraka kwa nchi hiyo ya Kiarabu iliyokumbwa na vita, ambapo mtoto mmoja hufariki dunia kila baada ya dakika kumi.

Taarifa iliyotolewa Ijumaa ya jana na UNICEF imesema kwamba "zaidi ya watoto 540,000 walio chini ya umri wa miaka mitano kati ya watoto milioni 11 wanaohitaji msaada wa kibinadamu nchini Yemen, wanakabiliwa na utapiamlo mbaya unaotishia maisha yao."

Taarifa hiyo imeongea kuwa: "Mtoto mmoja hufariki dunia (kwa wastani) kila baada ya dakika kumi kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika."

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema, linahitaji dola milioni 484 kwa mwaka huu wa 2023 ili kuendelea na shughuli zake katika nchi hiyo maskini zaidi kwenye Rasi ya Arabia, iliyoharibiwa na vita vya zaidi ya miaka minane vya Saudi Arabia na washirika wake.

Hadi sasa maelfu ya raia wasio na hatia yoyote wa Yemen wameuawa tangu muungano vamizi dhidi ya Yemen unaoongozwa na Saudia uanzisha vita nchini humo mwaka 2015.

Maelfu ya watoto wameuawa katika vita vya Saudia nchini Yemen

Wizara ya Haki za Binadamu ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen imetangaza kuwa: Idadi jumla ya raia waliouawa na kujeruhiwa katika kipindi cha miaka minane imepindukia elfu 49. Watoto zaidi ya 8,700 na wanawake zaidi ya 5,000 ni miongoni mwa raia wa Yemen waliouliwa vitani tangu kuanza vita vya muungano wa Saudia huko Yemen. 

Taarifa ya Wizara ya Haki za Binadamu ya Yemen imeongeza kuwa, katika kipindi chote hicho cha miaka minane, raia milioni moja na 483,000 pia wa Yemen wameaga dunia kwa njia isiyo ya moja kwa moja kulikosababishwa na maradhi ya kuambukiza, kuathirika na mada za kemikali za silaha zilizopigwa marufuku, utapiamlo na sababu nyingine mbalimbali.