Jordan yalaani upanuzi wa vitongoji vya walowezi unaofanywa na Israel
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jordan imelaani hatua ya utawala haramu wa Israel ya kujenga nyumba nyingine mpya zaidi ya 8,000 ikiwa ni katika mpango wa upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina.
Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jordan imesisitiza kuwa, hatua hiyo ya utawala vamizi wa Israel inakinzana wazi na haki za binadamu.
Sinan al-Majali, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jordan amesema kuwa, harakati za Israel za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni zinakinza wazi na sheria za kimataifa likiwemo azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la aUmoja wa Mataifa.
Azimio nambari 2234 la tarehe 23 Disemba 2016 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linataka kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.
Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.
Hivi majuzi mataifa 17 ya Ulaya ambayo mengi kati ya hayo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya sambamba na kukosoa sera za utawala ghasibu wa Israel yalitaka kuhitimishwa sera za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kufukuzwa familia za Kipalestina kutoka katika nyumba zao mashariki mwa Baytul-Muqaddas.