FAO: Mamilioni ya watu Afghanistan wako katika hatari ya njaa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i95636-fao_mamilioni_ya_watu_afghanistan_wako_katika_hatari_ya_njaa
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeonya kuhusu hatari ya njaa kwa mamilioni ya watu nchini Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 28, 2023 22:41 UTC
  • FAO: Mamilioni ya watu Afghanistan wako katika hatari ya njaa

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeonya kuhusu hatari ya njaa kwa mamilioni ya watu nchini Afghanistan.

Shirika la habari la Tasnim limeripoti kuwa, FAO imeonya kwamba iwapo watu wa Afghanistan hawatapokea msaada wa haraka katika siku zijazo, watu milioni 9 watafariki dunia kutokana na njaa katika nchi hiyo.

David Beasley, mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani, ameandika kwenye Twitter kwamba ulimwengu hauwezi kuwapa kisogo watu wa Afghanistan katika mgogoro wa sasa ambao haujawahi kutokea.

Hapo awali, Shirika la Kuratibu Misaada kwa Ajili ya Watu wa Afghanistan lilitangaza kwamba watu milioni 23 nchini humo wanapewa kipaumbele kwa ajili ya misaada ya kibinadamu, na kwamba Waafghani watasaidiwa ikiwa fedha za kutosha zinapatikana.

OCHA imeomba dola bilioni 4.6 kwa ajili ya kutoa msaada wa kibinadamu kwa watu wa Afghanistan.

Tahadhari ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa kuhusu hali mbaya ya upatikanaji wa chakula nchini Afghanistan imetolewa huku Marekani ikiendelea kuzuia mabilioni ya fedha za nchi hiyo kwa kutumia ubabe na mabavu.