Damascus: Tuko tayari kukabiliana na mashambulizi ya magaidi wa Israel
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imeyataja mashambulizi yaliyofanywa na ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi ya nchi hiyo kuwa ni ya kigaidi na kusisitiza kuwa, Damascus iko tayari kukabiliana na jinai hizo za kifashisti.
Ni baada ya Wizara ya Habari ya Syria kuthibitisha mapema jana Ijumaa (Machi 31) kwamba milipuko kadhaa ilisikika katika anga ya mji mkuu na viunga vyake.
Mfumo wa ulinzi wa jeshi la Syria umefanikiwa kuzuia makombora mengi ya adui Mzayuni katika anga ya Damascus. Jinai hii ni shambulio la pili la utawala wa Kizayuni dhidi ya Syria katika muda wa saa 24 na imelenga eneo la kusini mwa Damascus.
Ikizungumzia mashambulizi hayo ya utawala wa Kizayuni, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imesisitiza kwamba mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel dhidi ya Syria yanaonyesha uratibu wa karibu kati ya Tel Aviv na makundi ya kigaidi kwa lengo la kurefusha mgogoro ndani ya nchi hiyo.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesisitiza kuwa, Israel inaendelea kutekeleza siasa zake za vita na kutenda jinai dhidi ya Syria; na kwamba ndege za kivita za utawala huo zimeshirikiana kamili na makundi ya kigaidi yaliyoshambulia wanajeshi wa Syria katika eneo la Al-Dana na kufanya uhalifu mpya wa kikatili.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesema, mashambulizi hayo ya mara kwa mara yanaonyesha uratibu na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya magaidi wa Israel na makundi mengine ya kigaidi; na lengo lao ni kurefusha mgogoro wa Syria.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imeeleza kuwa, Damascus inathibitisha kuwa iko tayari kukabiliana na changamoto na mashambulizi ya kifashisti ili kutimiza matakwa ya watu wa Syria ya kuyashinda makundi ya kigaidi na kurejesha mamlaka ya Syria kwenye ardhi na anga yote ya nchi hiyo.