Yemen: Upumbavu wowote utakaofanywa na wavamizi tutaujibia ndani ya ardhi yao
Apr 02, 2023 07:21 UTC
Msemaji wa vikosi vya uinzi vya Yemen amesema: "iwapo wavamizi wa nchi hii watafanya upumbavu wowote ule, jibu letu litakuwa la kushtukiza na litajumuisha mashambulizi makubwa ambayo yataathiri eneo zima".
Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani, Muungano wa Falme za Kiarabu Imarati na nchi nyingine kadhaa, mnamo Machi 2015 iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, baharini na angani.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Saba, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesisitiza leo kwamba "wavamizi wa Yemen watashindwa tu; na kama tunavyoona, Waimarati hawapo tena kwenye medani ya vita bali wameishia kuwatumia maafisa wao wa mawasiliano tu kutokana na vipigo vikali na vya kutisha walivyopata".
Saree ameeleza kwamba, "lau kama vita vyetu vingekuwa na Wasaudi na Waimarati peke yao, vingemalizika katika mwaka uleule wa kwanza, lakini ushiriki wa Wayemen wenyewe katika uchokozi huu na kugeuzwa kuwa kuni za moto wa vita, kumepelekea kurefuka kwa vita hivi".
Brigedia Jenerali Saree amefafanua kuwa "Wasaudi na Waimarati hawawezi kuendelea kuikalia Yemen kwa mabavu milele, kwani Uingereza nayo ilikalia kwa mabavu kusini mwa nchi yetu kwa miaka 128, lakini mwishowe ililazimika kuondoka kwa fedheha na kimadhila".
Afisa huyo wa Yemen amesisitiza kuwa "muda wa uvamizi dhidi ya Yemen unakaribia mwishoni na vikosi vya ulinzi vya Yemen, kwa kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu, vimeazimia kwa dhati kuutimua nje ya nchi yao uvamizi wowote ule, na hii ndiyo ahadi tuliyotoa kwa uongozi wa Mapinduzi ya Yemen na watu wa nchi hii".
Saree ameendelea kueleza kwamba "ujumbe wetu kwa nchi vamizi ni kwamba kushindwa kwenu kutaendelea; na kwa kuwa hamjaweza kufikia lengo lenu kwa muda miaka minane, baadaye pia hamtaweza kulifikia".
Kituo cha haki za binadamu cha Yemen kimetangaza kuwa zaidi ya wanawake na watoto 13,000 wa Yemen wamekuwa wahanga wa uvamizi wa kijeshi wa miaka minane uliofanywa na muungano wa Saudia dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu.../