Wapalestina 2 wauawa shahidi, 16 wajeruhiwa huko Nablus
Shirika la Huduma za Dharura la Mwezi Mwekundu la Palestina limetangaza kuwa Wapalestina 2 wameuawa na 16 kujeruhiwa katika mapigano jana Jumatatu na wanajeshi wa utawala ghasibu wa Kizayuni huko Baita kusini mwa mji wa Nablus.
Mlolongo wa vitendo vya kiadui na uhasama vya wanajeshi wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ungali unaendelea, na kila siku wanashambulia maeneo tofauti ya Palestina ili kufikia malengo yao ya kujitanua huku wakiwauwa shahidi, kuwajeruhi na kuwatia mbaroni raia wasio na hatia wa Palestina.
Duru za habari zimearifu kuwa, mapigano makali yalijiri jana kati ya Wapalestina na wanajeshi wa Kizayuni karibu na eneo la kuingilia katika kitongoiji cha Yabad katika mji wa Jenin.
Katika upande mwingine, wanajeshi wa Kizayuni jana usiku waliuvamia msikiti wa al Aqsa na kujaribu kuwatoa ndani ya msikiti raia wa Palestina waliokuwa katika ibada. Wanajeshi hao wa Israel walijizatiti kwa silaha katika eneo la msikiti Mtakatifu wa al Aqsa.
Akijibu hujuma hiyo ya Wazayuni katika msikiti wa al Aqsa, Ekrima Sa'id Sabri Khatibu wa msikiti huo amesema: utawala ghasibu wa Kizayuni umeanza chokochoko zake za uwendawazimu dhidi ya msikiti Mtakatifu wa al Aqsa na kuendesha vita katika eneo hilo panapofanyika ibada ya Mwenyezi Mungu.