Israel yatenga $18M za ujenzi wa vitongoji vipya Palestina
Utawala haramu wa Israel umeidhinisha dola milioni 18 za Marekani zitakazotumiwa katika ujenzi wa vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina unazozikalia kwa mabavu.
David Keyes, msemaji wa Benjami Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amesema fedha hizo zimeidhinishwa na baraza la mawaziri la utawala huo kwa ajili ya kuendeleza ujenzi haramu katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Vyombo vya habari vya utawala huo ghasibu vimeripoti kuwa, fedha hizo ni sehemu ya dola milioni 88 za Marekani zilizoidhinishwa katika bajeti ya ziada ya utawala huo mwaka jana, kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu. Saeb Erekat, Katibu Mkuu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) ametaja hatua hiyo kama pigo katika uso wa jamii ya kimataifa. Amesema utawala wa Kizayuni unafanya kila jitihada kuvuruga mchakato wa haki na amani ya Palestina.
Haya yanajiri siku chache baada ya Riyad Mansour, Mwakilishi wa kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa kulitaka Baraza la Usalama la umoja huo kutekeleza majukumu yake na kuzuia ujenzi wa vitongoji zaidi vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.