Azma ya Pakistan ya kuanzisha operesheni dhidi ya makundi ya kigaidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i96160-azma_ya_pakistan_ya_kuanzisha_operesheni_dhidi_ya_makundi_ya_kigaidi
Baraza la Usalama wa Taifa la Pakistan chini ya uongozi wa Muhammad Shehbaz Sharif, Waziri Mkuu wa nchi hiyo limepasisha uamuzi wa kuendesha operesheni mpya dhidi ya ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 11, 2023 22:35 UTC
  • Azma ya Pakistan ya kuanzisha operesheni dhidi ya makundi ya kigaidi

Baraza la Usalama wa Taifa la Pakistan chini ya uongozi wa Muhammad Shehbaz Sharif, Waziri Mkuu wa nchi hiyo limepasisha uamuzi wa kuendesha operesheni mpya dhidi ya ugaidi.

Wajumbe wa Baraza la Usalama wa Taifa la Pakistan wameafiki katika kikao chao cha 41 cha kamati hiyo juu ya mpango wa operesheni mpya ya kijeshji ambayo ni jumuishi dhidi ya ugaidi hususan kwa ajili ya kukabiliana na changamoto zinazotokana na mashambulio ya kundi la kigaidi la Tehreek-e-Taliban-e-Pakistan, ambalo kimsingi linaendesha harakati zake katika mpaka wa nchi hiyo na Afghanistan, na limekuwa likihatarisha usalama wa raia katika maeneo hayo ya mpakani.

Iliafikiwa pia katika mkutano huo wa Baraza la Usalama wa Taifa la Pakistan uliohudhuriwa na makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Pakistan na wakuu wa vyombo vya kiintelijensia vya nchi hiyo ya kwamba, katika kipindi cha wiki mbili zijazo kuwe kumeshaundwa kamati ambayo itajumuisha maafisa wa ngazi za juu wa serikali na kijeshi ambayo itakuwa na jukumu muhimu la kuandaa sera na mikakati ya utekelezaji wa operesheni mpya za kijeshi.

Uamuzi huu umechukuliwa baada ya Pakistan kushuhudia katika miezi ya hivi karibuni kuongezeka na kushadidi wimbi la harakati za makundi ya kigaidi na yale yanayopigania kujienga katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, na hivyo kusikika kengele ya hatari.

Muhammad Shehbaz Sharif, Waziri Mkuu wa Pakistan

 

Licha ya kuwa, vyombo vya usalama vya Pakistan hivi karibuni vilimtia mbaroni mmoja wa vinara wa kundi linalopigania kujitenga la Balochistan Liberation Army na hivyo kutoa pigo kubwa kwa makundi yanayopigania kujitenga katika jimbo la Balochistan, lakini pamoja na hayo inaonekana kuwa, kile ambalo kina uharaka na kinapewa kipaumbele na serikali na jeshi la Pakistan ni kukabiliana na kundi la kigaidi la la Tehreek-e-Taliban-e-Pakistan ambalo hivi karibuni lilijiondoa katika makubaliano ya usitishaji mapigano na kuanza kufanya mashambulio dhidi ya jeshi la Pakistan. Hatua ya kundi hilo la kigaidi imeweka wazi msimamo wake ulio dhidi ya serikali ya Islamabad.

Mansur Ahmad Khan, mweledi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa ya Pakistan anasema kuhusiana na hilo kwamba: "Huenda jeshi la Pakistan katu halikuwa likidhani kwamba, ipo siku litakumbwa na jinamizi la makundi ya kigaidi ambayo wakati fulani ilikuwa ikituhumiwa kwamba, inayatumia makundi hayo kama wenzo wa kufikia malengo yake katika eneo.

Vyovyote itakavyokuwa, kimsingi harakati za makundi ya kigaidi hii leo ni moja ya changamoto zinazolikabili eneo la Asia Magharibi ambapo ili kukabiliana na changamoto hii kubwa na tishio, kuna haja ya kuweko ushirikiano wa kweli na wa dhati baina ya mataifa mbalimbali hususan kutoka upande wa Pakistan, ili kwa njia hiyo makundi hayo ya kigaidi yasiweze kufanya harakati zake kwa urahisi na hivyo kuyazuia yasihatarishe amani na usalama wa mataifa ya eneo.

 

Ala kulli haal, inaonekana kuwa, nchini Pakistan hakuna uratibu kamili baina ya vyombo vya mahakama, idara ya usalama, vyombo vya usalama, intelijensia na serikali. Hii ni kutokana na kuwa, akthari ya magaidi waliotiwa mbaroni huachiliwa kutoka kizuzini baada ya muda kwa kutumiwa sababu mbalimbali au hutoroka kutoka kifungoni. Inaelezwa kuwa, baadhi ya wanachama wa kundi la kigaidi la Tehreek-e-Taliban-e-Pakistan wameachiliwa huru kwa kisingizio cha kuhudhuria mazungumzo kati yao na serikali ya Islamabad ambapo hivi sasa hilo limegeuka na kuwa changamoto kubwa kwa usalama.

Kwa muktadha huo, wananchi wa Pakistan wanataraji kuona Idara ya Mahakama ikichukua hatua kali dhidi ya watu wanaotiwa mbaroni kwa makosa ya kigaidi akiwemo kinara wa kundi la Balochistan Liberation Army na hivyo kuthamini mchango wa vikosi vya usalama vya nchi hiyo Kwani kuchukua muda mrefu mwenendo wa kesi zao huwafanya watoroke kutoka kizuizini na akuzifanya juhudi za vikosi vya usalama kupotea bure.