Mazungumzo ya amani baina ya Yemen-Saudi yaanza kufanikiwa
Mjumbe mkuu wa harakati ya Ansarullah ya Yemen anasema mazungumzo ya amani baina ya nchi hiyo na Saudi Arabia yameanza kuzaa matunda na kwamba majadiliano zaidi yatafanyika ili kuondoa tofauti zilizosalia.
Pande hizo mbili zilihitimisha mazungumzo katika mji mkuu wa Yemen, Sana'a, siku ya jana Ijumaa, huku Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ikitangaza kuwa pande zinazozozana zimeanza mabadilishano ya karibu wafungwa 900.
Saudi Arabia inasema inataka makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano ili kumaliza vita dhidi ya Yemen ambavyo vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kuwaacha mamilioni ya watu wakisumbuliwa na njaa.
Ufalme wa Saudia unaongoza muungano ambao umekuwa ukiishambulia nchi hiyo masikini tangu 2015. Kulingana na wanadiplomasia wa Kiarabu, hivi sasa Saudi Arabia inataka kujiondoa katika kinamasi cha vita nchini Yemen.
Ziara ya wajumbe wa Saudia mjini Sana'a iliashiria nia ya kuendeleza mapatano yaliyokwisha muda wake ya Umoja wa Mataifa.
Mjumbe mkuu wa Ansarullah katika mazungumzo, Mohammed Abdulsalam amesema kwamba mazungumzo na wajumbe kutoka Saudi Arabia na Oman, yamekuwa "ya kina na chanya".
Katika ujumbe wake kupitia ukurasa wa Twitter amesema: "Kuna maendeleo katika baadhi ya masuala na kuna matumaini ya kutatuliwa masuala mengine baada ya uchunguzi."
Mazungumzo hayo yanaripotiwa kulenga suala la kusitisha mapigano, kufungua tena kikamilifu bandari za kusini na uwanja wa ndege wa Sana'a, malipo ya mishahara ya sekta ya umma, juhudi za kuijenga upya nchi hiyo, na kuondoka vikosi vya askari wa kigeni nchini Yemen.
Ansarullah na washirika wake wanashikilia mamlaka kaskazini mwa Yemen.
Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa, harakati hiyo imekubali kuwaachilia wafungwa 181 wakiwemo wanajeshi wa Saudia na Sudan ambao walikamatwa katika vita vilivyoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen kwa msaada wa kijasusi Marekani na madola mengine ya Magharibi.
Wafuatiliaji wa mambo wanaamini kuwa maelewano ya hivi majuzi kati ya Iran na Saudi Arabia yanaweza kusaidia kuimarisha utulivu na amani katika eneo la Asia Magharibi, na hivyo kurahisisha juhudi za kufikia amani endelevu Yemen.