Yemen: Mabadilishano makubwa ya wafungwa yaleta matumaini ya kuhimitimisha vita
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i96318-yemen_mabadilishano_makubwa_ya_wafungwa_yaleta_matumaini_ya_kuhimitimisha_vita
Mabadilishano makubwa ya wafungwa kati ya pande zinazozozana nchini Yemen yanaendelea, ambayo yanaonekana kama sehemu ya juhudi za kumaliza vita vya Yemen vilivyodumu kwa zaidi ya miaka minane sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 15, 2023 22:15 UTC
  • Yemen: Mabadilishano makubwa ya wafungwa yaleta matumaini ya kuhimitimisha vita

Mabadilishano makubwa ya wafungwa kati ya pande zinazozozana nchini Yemen yanaendelea, ambayo yanaonekana kama sehemu ya juhudi za kumaliza vita vya Yemen vilivyodumu kwa zaidi ya miaka minane sasa.

Maafisa wa Msalaba Mwekundu wametangaza kuwa, wafungwa 318 wamesafirishwa kwa ndege nne kati ya Sanaa mji mkuu unaodhibitiwa na Harakati ya Ansarullah na Aden. Takriban wafungwa 900 wanatarajiwa kubadilishana kwa muda wa siku tatu zijazo. Mabadilishano hayo  makubwa zaidi tangu mwishoni mwa mwaka 2020  yanaonekana kama hatua ya kujenga imani, kufuatia mazungumzo mapema wiki hii mjini Sanaa kati ya ujumbe wa Saudi Arabia na Harakati ya Ansarullah.

Saudi Arabia inasema inataka makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano ili kumaliza vita dhidi ya Yemen ambavyo vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kuwaacha mamilioni ya watu wakisumbuliwa na njaa.

 

Ufalme wa Saudia unaongoza muungano ambao umekuwa ukiishambulia nchi hiyo masikini tangu 2015. Kulingana na wanadiplomasia wa Kiarabu, hivi sasa Saudi Arabia inataka kujiondoa katika kinamasi cha vita nchini Yemen.

Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa, harakati hiyo imekubali kuwaachilia wafungwa 181 wakiwemo wanajeshi wa Saudia na Sudan ambao walikamatwa katika  vita vilivyoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen kwa msaada wa kijasusi Marekani na madola mengine ya Magharibi.

Wafuatiliaji wa mambo wanaamini kuwa maelewano ya hivi majuzi kati ya Iran na Saudi Arabia yanaweza kusaidia kuimarisha utulivu na amani katika eneo la Asia Magharibi, na hivyo kurahisisha juhudi za kufikia amani endelevu Yemen.