Haniya: Taifa la Palestina halina njia nyingine isipokuwa muqawama na mapambano
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i96328-haniya_taifa_la_palestina_halina_njia_nyingine_isipokuwa_muqawama_na_mapambano
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesisitiza juu ya umoja katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kueleza kwamba, taifa la Palestina halina njia nyingine ya kuwatimua wavamizi isipokuwa kuendeleza muqawama, uthabiti na mapigano.
(last modified 2026-07-31T06:29:55+00:00 )
Apr 16, 2023 03:27 UTC
  • Haniya: Taifa la Palestina halina njia nyingine isipokuwa muqawama na mapambano

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesisitiza juu ya umoja katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kueleza kwamba, taifa la Palestina halina njia nyingine ya kuwatimua wavamizi isipokuwa kuendeleza muqawama, uthabiti na mapigano.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina Sama, Ismail Haniya amesema Hamas inapiga hatua katika pande tatu ili kuendana na mabadiliko ya kimkakati katika ngazi ya ndani, kikanda na kimataifa, ambapo katika mwelekeo wa kwanza ni kujiweka tayari muda wote kwa mapambano; mwelekeo wa pili ni kuanzisha umoja wa kweli na njia na muelekeo wa tatu ni kuimarisha ushirikiano na mashauriano na ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.
Haniya ameongeza kuwa, baada ya zaidi ya miongo saba ya kukaliwa ardhi zake kwa mabavu, imethibitika kuwa bila shaka yoyote taifa la Palestina litaendelea kubaki na dhana hewa ya kulifuta kwenye ramani ni kitu muhali, na vizazi vipya vya Wapalestina ndani na nje ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu vinazidi kupigania kurejesha haki zao.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Hamas amesema, katika mazingira ya kuwepo baraza la mawaziri hatari zaidi la Wazayuni na lenye misimamo mikali zaidi ya kufurutu mpaka taifa la Palestina halina njia nyingine isipokuwa kuendeleza muqawama na uthabiti na kupambana hadi litakapowafurusha wavamizi hao.

Haniyah amesisitiza kuwa taifa lililovamiwa na kukaliwa kwa mabavu halitakomboka isipokuwa kwa kuwa na  umoja, na Hamas iko tayari kufanya lolote lile ili kupatikana umoja huo.
Aidha ametoa wito wa kuwekewa mzingiro wa kisiasa baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni na kulibana lisiweze kuendesha harakati zake hususan katika eneo la Kiarabu na Kiislamu.../