Wapalestina 24 watiwa nguvuni huko Quds na Ukingo wa Magharibi
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameshambulia baadhi ya maeneo katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na utawala huo na katika Ukingo wa Magharibi na kuwatia nguvuni Wapalestina 24.
Maghasibu wa Kizayuni katika wiki za hivi karibuni hasa katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani wamezidisha hujuma na mashambulizi dhidi ya raia wa Palestina huku wakiwatia mbaroni baadhi yao.
Tokea kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani hadi sasa wanajeshi wa utawala haramu wa Israel wamewata nguvuni zaidi ya Wapalestina 450 katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.
Televisheni ya Palestine al Yaum imeripoti kuwa Wazayuni leo Jumapili wamewatia mbaroni vijana watatu wa Kipalestina baada ya kushambulia eneo la Babul Harah huko Quds inayokaliwa kwa mabavu.
Taasisi za haki za binadamu za Palestina zimetangaza kuwa hivi sasa mateka wa Kipalestina walioko katika jela za utawala wa Kizayuni wamefikia karibu 4,900.
Aidha utawala wa Kizayuni unashikilia miili ya mateka 12 wa Kipalestina walioaga dunia na umekataa kukabidhi miili hiyo kwa familia zao.