Iraq: Tunapinga kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel
Mohammed al-Halbousi, Spika wa Bunge la Iraq amesisitiza kuwa, nchi yake inapinga vikali kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel unaotenda jinai kila leo dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Spika wa Bunge la Iraq amesema hayo mjini Baghdad katika mazungumzo yake na Ziyad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina na kusisitiza tena msimamo wa nchi yake wa kuliunga mkono taifa la Palestina.
Kadhalika Spika al-Halbousi amesema, msimamo rasmi na wa wananchi wa Iraq ni kuliunga mkono taifa madhulumu la Palestina na haki yake ya kuendesha mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.
Mwaka jana Bunge la Iraq lilipasisha kwa kauli moja sheria ya kupiga marufuku ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Kwa mujibu wa Bunge la Iraq, sheria hiyo kuanzisha uhusiano na Israel kunatambuliwa na katiba ya nchi hiyo kuwa ni uhalifu na inatoa adhabu ya kifo kwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kuhusika na uhalifu huo.
Mwaka 2020 nchi nne za Kiarabu za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Bahrain, Morocco na Sudan zilianzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu unaoendelea kuikalia kwa mabavu Quds Tukufu, hatua ambayo imeendelea kukosolewa na kulalamikiwa vikali.
Maandamano yamekuwa yakishuhudiwa mara kwa mara katika mataifa hayo kkuulalamikia hhatua ya tawala zao ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel.