Al-Houthi: Muungano wa Saudia ndio uliohusika na maafa ya Sana'a
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i96502-al_houthi_muungano_wa_saudia_ndio_uliohusika_na_maafa_ya_sana'a
Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen ameutuhumu muungano wa vita unaoongozwa na Saudi Arabia kuwa ndio uliohusika na vifo na majeruhi ya makumi ya raia wa Yemen kutokana na msongamano wa watu mjini Sana'a.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 21, 2023 03:51 UTC
  • Al-Houthi: Muungano wa Saudia ndio uliohusika na maafa ya Sana'a

Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen ameutuhumu muungano wa vita unaoongozwa na Saudi Arabia kuwa ndio uliohusika na vifo na majeruhi ya makumi ya raia wa Yemen kutokana na msongamano wa watu mjini Sana'a.

Ni baada ya Watu zaidi ya 80 kupoteza maisha na mamia kujeruhiwa huko Yemen katika mkanyagano uliotokea jana katika zoezi la ugavi wa msaada wa hisani wa mfanyabiashara mmoja.

Mohammed Ali Al-Houthi, mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Tukio la msongamano wa watu ni janga chungu, msiba mpya na picha mbaya, ambayo kimsingi imesababishwa na muungano wa Marekani, Uingereza, Saudi na Imarati na washirika wao."

Al-Houthi amesema muungano wa Saudia umewaweka watu wa Yemen katika mzozo mbaya zaidi wa kimataifa na wa binadamu, na zaidi ya hayo, waliokuwa wakigawa msaada hawakutumia njiia za busara na mantikki katika kugawa misaada hiyo.

Mjumbe huyo wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amezishutumu nchi vamizi kuwa zimehusika na tukio hilo chungu na kuongeza kuwa, watu wa Yemen wamekumbwa na maafa hayo  kutokana na uvamizi, vikwazo na kukatiwa mishahara.

Mkanyagano huo ulitokea jana katika nchi masikini ya Kiarabu ya Yemen siku moja kabla ya baadhi ya Waislamu duniani kusherehekea Sikukuu ya Idul-Fitr baada ya kukamilisha funga ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani. 

Habari zinasema kuwa mamia ya watu walikusanyika katika shule moja mjini Sana'a, mji mkuu wa Yemen, kwa ajili ya kupokea msaada wa fedha wa Riali 5,000 za Yemen sawa na dola 8 za Marekani.  

Watu wasiopungua 85 wamepoteza maisha na zaidi ya 322 wamejeruhiwa katika mkanyagano uliotokea kwenye zoezi hilo la hisani katika wilaya ya Babul Yemen huko Sana'a. Wanawake na watoto ni miongoni mwa wahanga wa ajali hiyo. Wizara ya Afya ya Yemen imeripoti kuwa, watu waliohusika na tukio hilo wamekamatwa.