Bahrain kumvua uraia Sheikh Qassim ni njama ya Saudia
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran, IRGC limetoa taarifa na kulaani hatua ya utawala wa kiimla wa Bahrain wa kumvua uraia mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Isa Qassim na kusema hatua hiyo ilipangwa na utawala wa Saudia.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kwa hatua hiyo, utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain umeonyesha kutokuwa na ubinadamu na namna ulivyo na misimamo ya kibaguzi na kiu ya damu. Aidha taarifa hiyo imesema hatua hiyo ya Aal Khalifa ni kinyume cha haki za kiraia, misingi ya Uislamu, kanuni za kimataifa na hadhi ya watu wa nchi za Kiarabu.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran limebaini kuwa, kumvua uraia Sheikh Qassim ni natija ya stratijia za njama dhidi ya Uislamu, sera za madola ya kibeberu na Kizayuni na njama ya Saudia.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, hatua hiyo isiyo na busara ya ukoo wa Aal Khalifa dhidi ya mwanazuoni wa ngazi za juu wa Kishia ni jambo ambalo litaupa nguvu mwamko na mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi wa Bahrain.
Siku ya Jumatatu, Bahrain ilimvua uraia Sheikh Qassim kwa tuhuma zisizo na msingi kuwa eti anachochea malumbano ya kimadhehebu na ghasia. Sheikh Qassim ni mashuhuri kwa misimamo yake ya kutetea Umoja wa Kiislamu na maandamano ya amani Bahrain.