Saudi Arabia na Syria zatangaza uamuzi wa kurejesha uhusiano wa kidiplomasia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i97188-saudi_arabia_na_syria_zatangaza_uamuzi_wa_kurejesha_uhusiano_wa_kidiplomasia
Saudi Arabia na Syria zimetangaza uamuzi wa kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia, baada ya kupita zaidi ya muongo mmoja tangu Riyadh ilipochukua hatua ya kuvunja uhusiano huo na kuanza kuunga mkono makundi ya kigaidi yaliyokuwa yakipambana na serikali ya Damascus.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2023 03:07 UTC
  • Saudi Arabia na Syria zatangaza uamuzi wa kurejesha uhusiano wa kidiplomasia

Saudi Arabia na Syria zimetangaza uamuzi wa kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia, baada ya kupita zaidi ya muongo mmoja tangu Riyadh ilipochukua hatua ya kuvunja uhusiano huo na kuanza kuunga mkono makundi ya kigaidi yaliyokuwa yakipambana na serikali ya Damascus.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudia iliyonukuliwa na shirika la habari la nchi hiyo imesema, utawala huo wa kifalme "umeamua kuanzisha tena shughuli za ujumbe wake wa kidiplomasia nchini Syria".

Kwa upande wa Syria, shirika rasmi la habari la nchi hiyo SANA limemnukuu afisa katika Wizara ya Mambo ya Nje akisema, "Jamhuri ya Kiarabu ya Syria imeamua kuanzisha tena shughuli za ujumbe wake wa kidiplomasia nchini Saudi Arabia".

Wiki tatu zilizopita, Rais Bashar al-Assad wa Syria alikutana mjini Damascus na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan, ikiwa ni ziara ya kwanza ya aina yake kufanywa na afisa wa ngazi ya juu wa Riyadh nchini Syria tangu mwaka 2011.

Rais Bashar al-Assad wa Syria (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudia Faisal bin Farhan

Kwa mujibu wa taarifa ambayo ilitolewa na wizara ya mambo ya nje ya Saudia baada ya mazungumzo hayo, Assad na Faisal walijadili hatua za "kufikia suluhu ya kina ya kisiasa ambayo... itachangia kurejea Syria kwenye kambi ya Waarabu".

Siku ya Jumapili, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilikubaliana kupitia uamuzi uliotangazwa na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama kurejeshwa uanachama wa Syria katika taasisi hiyo kuu ya mataifa ya Kiarabu.

Itakumbukwa kuwa Saudi Arabia na washirika wake walivunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Syria mwaka 2011 kufuatia kuzuka wimbi kubwa la machafuko na mapigano yaliyoanzishwa na makundi ya kigaidi yakichochewa na kuungwa mkono na muungano wa Magharibi na wa Waarabu dhidi ya taifa hilo la Kiarabu.../