Syria yaifukuza BBC kuripoti katika ardhi ya nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i99704-syria_yaifukuza_bbc_kuripoti_katika_ardhi_ya_nchi_hiyo
Serikali ya Syria imetangaza kuwa imebatilisha kibali cha shirika la habari la Uingereza, BBC kutokana na kutoa ripoti za kupotosha.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Jul 09, 2023 04:44 UTC
  • Syria yaifukuza BBC kuripoti katika ardhi ya nchi hiyo

Serikali ya Syria imetangaza kuwa imebatilisha kibali cha shirika la habari la Uingereza, BBC kutokana na kutoa ripoti za kupotosha.

Wizara ya Habari ya Syria imesema katika taarifa yake kwamba kutokana na BBC kushindwa kuzingatia viwango vya kitaaluma na kuendelea kwake kutoa ripoti za kisiasa na za kupotosha, imeamuliwa kubatilisha kibali cha mwandishi na mpiga picha wa shiriika hilo.

Wizara ya Habari ya Syria imesema kwamba tangu kuzuka kwa vita mwaka 2011, "televisheni ya BBC imekuwa ikitoa kwa makusudi, na mara kwa mara, habari na ripoti za uongo kuhusu hali ya Syria.

Wizara hiyo iliongeza kuwa "televisheni hiyo ilitahadharishwa zaidi ya mara moja, lakini iliendelea kutangaza ripoti zake za kupotosha kwa kutegemea taarifa za makundi ya kigaidi."

Mwezi uliopita BBC ilichapisha ripoti juu ya kile ilichodai ni "mahusiano ya moja kwa moja" kati ya biashara ya Captagon na familia ya Rais wa Syria, Bashar al-Assad, pamoja na jeshi la serikali ya nchi hiyo.

Marekani, na baadhi ya washirika wake wa Ulaya wanautuhumu utawala wa Syria kuwa unazalisha na kuuza nje dawa hiyo ya kulevya, na kumtaja Maher al-Assad, kamanda wa Kitengo cha Nne katika jeshi na kaka wa rais wa utawala huo, kuwa ni mmoja wa wahusika wakuu wanaohusika katika biashara hiyo.