Maafisa wa UN washtushwa na uharibifu uliotekelezwa na Israel huko Jenin
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i99766-maafisa_wa_un_washtushwa_na_uharibifu_uliotekelezwa_na_israel_huko_jenin
Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa na washirika wafadhili Jumapili walitembelea kambi ya wakimbizi wa Kipalestina katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Ukingo wa Magharibi wa Jenin, ambapo wameshuhudia uharibifu wa kushtua uliofanyika wakati wa uvamizi wa utawala haramu wa Israeli wiki iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 11, 2023 01:05 UTC
  • Maafisa wa UN washtushwa na uharibifu uliotekelezwa na Israel huko Jenin

Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa na washirika wafadhili Jumapili walitembelea kambi ya wakimbizi wa Kipalestina katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Ukingo wa Magharibi wa Jenin, ambapo wameshuhudia uharibifu wa kushtua uliofanyika wakati wa uvamizi wa utawala haramu wa Israeli wiki iliyopita.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, operesheni hiyo ya kijeshi ya siku mbili ndiyo kali zaidi katika kipindi cha miaka 20,

Takriban Wapalestina 12 waliuawa shahidi, wakiwemo watoto wanne, na wengine 140 walijeruhiwa na pia takriban nyumba 900 ziliharibiwa, na nyingi sasa haziwezi kukalika tena.

Leni Stenseth, naibu kamishna mkuu wa UNRWA, amesema "Tumekwenda kwenye kambi ya Jenin na washirika wetu kuonyesha mshikamano na wakaazi na kuwahakikishia kuwa hawako peke yao."

Ujumbe huo pia ulijumjumuisha Adam Bouloukos, mkurugenzi wa ofisi ya Ukingo wa Magharibi wa shirika hilo, na Lynn Hastings, mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa na wa misaada ya kibinadamu. 

Waliandamana pia na wawakilishi kadhaa wakuu kutoka jumuiya ya kimataifa na wafadhili.

Bi Stenseth  ameongeza kuwa "Uharibifu niliouona ulikuwa wa kushangaza. Baadhi ya nyumba ziliteketea kabisa, magari yalikuwa yamesambaratishwa kwa kuta, barabara zimeharibiwa, kituo cha afya cha UNRWA kimeharibiwa pia. Lakini, zaidi ya uharibifu wa kimwili, nimeona kiwewe machoni pa wakazi wa kambi ambao walikuwa wameshuhudia vurugu. Nimewasikia wakizungumza kuhusu uchovu na woga wao.”

Hali baada ya utawala katili wa Israel kutekeleza hujuma dhidi ya Jenin

Kwa mujibu wa UNRWA takriban watu 24,000 wanaishi katika Kambi ya Wakimbizi ya Jenin, ambayo iko kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi. 

Kituo cha afya cha UNRWA hapo kimeharibiwa vibaya kiasi kwamba hakiwezi kutumika tena, na shule zake nne zilipata uharibifu mdogo, shirika hilo limesema.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limewataka wafadhili na washirika kutoa fedha mara moja kwa ajili ya kutekeleza hatua zake za kibinadamu katika kambi hiyo.

Bi. Stenseth pia amesisitiza hitaji kubwa la amani katika maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu "kupitia suluhisho la kisiasa linalohitajika sana ambalo pia litashughulikia changamoto ya wakimbizi wa Kipalestina".