Wasiwasi kuhusu ukatili wa Israel dhidi ya watoto Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i9982-wasiwasi_kuhusu_ukatili_wa_israel_dhidi_ya_watoto_wapalestina
Kufuatia kushadidi ukatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watoto Wapalestina, kumekuwepo wasiwasi na malalamiko makubwa miongoni mwa Wapalestina na jamii ya kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 26, 2016 02:50 UTC
  • Wasiwasi kuhusu ukatili wa Israel dhidi ya watoto Wapalestina

Kufuatia kushadidi ukatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watoto Wapalestina, kumekuwepo wasiwasi na malalamiko makubwa miongoni mwa Wapalestina na jamii ya kimataifa.

Kuhusiana na hili, Farhan Haq, Msemaji wa Umoja wa Mataifa, jana Jumamosi aliashiria ukatili wa utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina na kusema umoja huo utachunguza ukatili wa Israel hasa dhidi ya watoto.

Farhan Haq amesema umoja huo utachunguza kifo cha Mahmoud Badran,kijana mdogo Mpalestina aliyekuwa na umri wa miaka 15 na ambaye alikufa shahidi hivi karibuni baada ya kufyatuliwa risasi na mwanajeshi wa utawala haramu wa Israel. Mwanajeshi aliyetekeleza ukatili huo amedai kuwa alifanya hivyo bila kukusudia.

Katika miezi ya hivi karibuni tumeshuhudia kuongezeka ukatili wa Israel dhidi ya watoto Wapalestina ambapo takwimu zinaonyesha ongezeko kubwa la watoto Wapalestina wanaouawa,kujeruhiwa au kutekwa nyara na utawala wa Israel ambao moja ya sifa zake kuu ni muuaji watoto.

Mashirika ya kimataifa yamekuwa yakifichua jinai za kuogofya zinazotekelezwa na utawala haramu wa Israel jambo ambalo linazidi kuwakasirisha walimwengu na kuongeza chuki dhidi ya utawala huo dhalimu.

Kile kilicho wazi ni kuwa, hatua za Israel katika kuwaua kiholela Wapalestina ni mfano wa wazi kabisa wa jinai dhidi ya binadmau na mauaji ya kimbari. Ukatili huo wa Israel unazidi kuumiza nyoyo za walimwengu.

Hatua ya utawala wa Kizayuni ya kukiuka misingi ya ubinadamu na haki za Wapalestina ni jambo ambalo limewabainishia walimwengu kuhusu namna Israel ilivyo na utambulisho ulio dhidi ya ubinadamu.

Mienendo ya utawala wa Kizayuni ni thibitisho la namna utawala huo ghasibu usivyojali chochote wakati wa kutekeleza jinai zake. Utawala haramu wa Israel unaendeleza jinai dhidi ya Wapalestina huku ukipata uungaji mkono wa madola ya Magharibi na hata baadhi ya tawala saliti za Kiarabu.

Utawala wa Kizayuni wa Israel unaongoza katika tawala zenye kukiuka sheria za kimataifa kuhusu watoto. Utawala huo mbali na kuwaua kinyama watoto wadogo, pia huwakamata, kuwatesa na kuwafunga katika magereza ya kuogofya. Hivi sasa kuwaua watoto Wapalestina ni jambo la kawaida miongoni mwa wanajeshi wa Israel. Ni nadra siku ipite bila wanajeshi wa Israel kutekeleza vitendo vya unyama, ukatili na mauaji ya watoto Wapalestina.

Unyama na ukatili wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watoto ni kinyume cha sheria za kimataifa hasa Ibara ya 16 ya Hati ya Haki za Watoto.

Hii ni katika hali ambayo, utawala wa Israel, ambao unakalia Quds Tukufu kwa mabavu, haukuwekwa katika orodha ya Umoja wa Mataifa ya tawala zinazokiuka haki za watoto. Ni wazi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyetayarisha orodha hiyo amepuuza ukatili wa Israel.

Kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni hasa dhidi ya watoto Wapalestina na hatua ya Umoja wa Mataifa ya kutosheka tu na kutoa takwimu au kulaani kwa maneno matupu yasiyo na maana jinai hizo ni jambo ambalo litapelekea walimwengu kuendelea kushuhudia, kwa masikitiko makubwa, ukatili wa utawala huo haramu dhidi ya watoto wa Kipalestina.