Ansarullah yatahadharisha kuhusu taathira za kiuchumi za kuendelea mzingiro Yemen
Msemaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen ametahadharisha kuhusu taathira za kiuchumi za kuendelea kuzingirwa nchi hiyo na muungano vamizi wa Saudia.
Vita vya Saudia dhidi ya Yemen kwa uungaji mkono wa Marekani, Imarati (UAE) na nchi nyingine kadhaa vilivyoanza tokea Machi 2015 vimewasababishia wananchi wa Yemen hasara na maafa makubwa. Vita hivyo pia vimeua mamia ya maelfu ya wananchi wa Yemen na kusababisha hasara ya kiuchumi ya makumi ya mabilioni ya dola.
Muhammad Abdulsalam jana usiku alisema kuwa vikosi vamizi vinapasa kusitisha hatua zote zinazowalenga wananchi wa Yemen na kuathiri mahitaji muhimu ya maisha ya raia hao.
Mkuu wa ujumbe wa timu ya mazungumzo ya serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen ameongeza kuwa, wenzo wa kiuchumi wa kufikia malengo ya kijeshi na kisiasa unapasa kuwekwa kando ili kupunguza masaibu yanayowakabili wananchi wa Yemen. "Mapato ya mafuta na gesi yatengwe ili kushughulikia matatizo ya kiuchumi ya wananchi na hasa kulipa mishahara ya wafanyakazi," amesema Muhammad Abdusalam.