Uchunguzi: Ukraine imekuwa makaburi ya silaha na zana za kivita ya NATO
-
Vifaru aina ya Leopard 2 vya Wajerumani vilivyoharibiwa, Ukraine
Takwimu na ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, Ukraine imegeuzwa makaburi ya silaha na zana za kivita za nchi wanachama wa shirika la kijeshi la nchi za Magharibi, NATO.
Tangu kuanza kwa vita vya Ukraine na Russia, medani na maeneo ya vita yamegeuka kuwa makaburi ya silaha na zana za kivita zinazotumwa kwa wingi na nchi wanachama wa NATO kwa serikali ya Kiev inayopigana na Russia katika vita vya niaba.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Kiev ilitangaza miezi kadhaa iliyopita kwamba imeanzisha jitihada kubwa za kukomboa maeneo yaliyotwaliwa, lakini juhudi hizo hazijafua dafu, na zana na silaha za nchi za Magharibi zilizoharibiwa zinaonekana kila mahali.
Maafisa wa serikali ya Ukraine wametangaza kuwa uhaba wa vifaa na zana za kivita ndiyo sababu ya kushindwa kwao, huku uimara wa jeshi Russia, ambalo lilikuwa limejitayarisha kwa ajili ya vita kwa muda mrefu, pia ukiwa sababu nyingine ya kushindwa kwa jeshi la Ukraine.
Wataalamu wanasema, silaha na vifaa vya nchi za Magharibi vimekuwa shabaha rahisi kwa jeshi la Russia, na uwanja wa vita umegeuka kuwa makaburi ya zana za kivita za NATO.
Sambamba na hayo, Umoja wa Ulaya umepuuza maombi ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy ya kuitishwa mkutano wa umoja huo utakaoshirikisha wakuu wa nchi za Amerika Kusini.