Moscow yasisitiza kuwa itatimiza malengo yake ya kijeshi huko Ukraine
Dmitry Medvedev, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia, amesema kuwa nchi yake ina vikosi vya jeshi vya kutosha kutekeleza majukumu yote ya operesheni maalumu ya kijeshi nchini Ukraine.
Dmitry Medvedev, amesema kuwa nchi yake ina nguvu na uwezo wa kijeshi wa kutosha wa kutimiza malengo yote ya operesheni zake za kijeshi nchini Ukraine na kurejesha amani katika nchi hiyo kwa mujibu wa masharti yake, na kusisitiza kuwa maadui wote wa Russia katika nchi za Magharibi zitakandamizwa.
Akikumbusha kuwa miaka 15 iliyopita, Moscow ilijibu ipasavyo shambulio la kikatili dhidi ya mji wa Tskhinvali, mji mkuu wa Jamhuri ya Ossetia Kusini, Naibu Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia amesema kwamba, kama ilivyokuwa mwezi Agosti 2008, maadui watagandamizwa, na Russia itafanya suluhu na amani kwa masharti yake yenyewe.
Dmitry Medvedev amesema kuwa mfumo mzima wa shirika la kijeshi la NATO uko vitani na Russia, na kwamba mzozo wa Ukraine ni matokeo ya jaribio la Marekani la kushambulia tena Russia.
Wakati huo huo, taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema kuwa wanajeshi wapatao 700 wa Ukraine wameuawa wakati wa operesheni za kijeshi za Russia nchini Ukraine katika muda wa saa 24 zilizopita.