Aug 15, 2023 03:30 UTC
  • UN yalaani shambulizi la kigaidi mjini Shiraz, kusini mwa Iran

Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani shambulio la kigaidi katika haram ya Sayyid Ahmad Bin Musa (as) maarufu kama Shah Cheragh katika mji wa Shiraz mkoani Fars, kusini mwa Iran.

Akijibu suali la mwandishi wa habari wa IRNA mjini New York kuhusu tukio hilo, Dujarric amesema  Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN amelaani vikali shambulio hilo la kigaidi dhidi eneo la kidini la Shah Cheragh.

Amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatoa mkono wa pole na anaungana na wananchi na serikali ya Iran kuomboleza, kufuatia shambulio hilo la juzi Jumapili, ambalo ni la pili la aina hiyo dhidi ya eneo hilo tukufu ndani ya miezi 10.

Habari zaidi zinasema kuwa, Umoja wa Ulaya pia umetoa taarifa ya kulaani hujuma hiyo ya kigaidi iliyolenga raia wasio na hatia wakiwa ndani ya eneo takatifu la kidini.

UN na EU zimetoa taarifa hizo baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kusema kuwa, kimya cha jamii ya kimataifa na nchi zinazodai kutetea haki za binadamu baada ya hujuma za kigaidi nchini Iran ni jambo ambalo linahimiza ugaidi.

Hadi sasa, mtu mmoja ameripotiwa kuuawa shahidi katika tukio hilo la kigaidi na wengine wanane wamejeruhiwa. Gaidi aliyehusika wa shambulizi hilo alikamatwa na maafisa wa usalama na polisi waliofika kwa wakati. Aidha washukiwa wengine wanne wamekamatwa hadi sasa kwa tuhuma za kuhusika na shambulio hilo la kigaidi.

Vyombo vya habari vimeripoti kwamba, magaidi wawili walihusika katika ufyatuaji risasi huo siku ya Jumapili. Mmoja wa washambuliaji anasemekana kuwa ametoroka. Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh limedai kuhusika na hujuma hiyo mbaya.

Ikumbukwe kuwa, mnamo Oktoba 26, 2022, gaidi mwenye silaha aliingia ndani ya eneo hilo la ibada, na kuwaua wafanyaziara 15, wakiwemo wanawake na watoto, na kujeruhi wengine kadhaa kabla ya kupigwa risasi na kujeruhiwa na vikosi vya usalama. Gaidi huyo baadaye alifariki hospitalini kutokana na majeraha aliyopata.

Tags