Qur'ani yachomwa tena Sweden; Waislamu na Wakristo waandamana
Kwa mara nyingine tena, kafiri Salwan Momika, mkimbizi wa Iraq anayeishi nchini Sweden ameivunjia heshima Qur'ani Tukufu mjini Stockholm chini ya himaya ya polisi ya nchi hiyo ya Ulaya.
Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Momoka akisaidiwa na kafiri mwenzake Salwan Najem mwenye asili ya Iraq pia, wamekanyaga na kuchoma moto nakala za Kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu mbele ya Bunge la nchi hiyo mjini Stockholm.
Duru za habari zinaarifu kuwa, polisi ya Sweden imewatia mbaroni wanaharakati kadhaa waliojaribu kusimamisha uafriti huo wa kuivunjia heshima na kuidhalilisha Qur'ani Tukufu.
Wakati huo huo, Waislamu na Wakristo ambao wameishi kwa utangamano kwa miaka mingi wamefanya maandamano ya amani katika eneo la Fisksatra, viungani mwa mji mkuu wa Swden, Stockholm kulaani wimbi hilo la kuvunjia heshima matukufu ya kidini nchini humo.
Haya yanajiri siku chache baada ya wanachama wa kundi la wabaguzi wa rangi linalojiita Wazalendo wa Denmark kuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu mbele ya ubalozi wa Uturuki. Wanachama wa kundi hilo pia walichoma moto nakala nyingine ya Qur'ani mbele ya ubalozi wa Iraq mjini Copenhagen.
Dharau na vitendo vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Sweden na Denmark vimeongezeka sana katika wiki za hivi karibuni, na vimekabiliwa na malalamiko katika nchi za Waislamu na kwenye duru za kimataifa.
Nchi za Magharibi zinaruhusu kutukana na kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu, hasa kuchoma moto Qur'ani Tukufu kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza.