Aug 19, 2023 10:28 UTC
  • Waislamu waghadhabishwa na kuchomwa moto Qur'ani Uholanzi

Waislamu katika kona zote za dunia wamehamakishwa na kitendo kingine cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu, mara hii katika mji wa The Hague nchini Uholanzi.

Waislamu wa matabaka yote hasa vijana katika mitandao ya kijamii wamelaani vikali wimbi hilo la kuvunjia heshima matukufu ya kidini katika nchi za Magharibi, baada ya Waholanzi wenye misimamo mikali kuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu nje ya ubalozi wa Uturuki mjini Hague.

Polisi ya Uholanzi imewashambuliwa na kuwakamata baadhi ya Waislamu waliokusanyika nje ya ubalozi huo kulalamikia kitendo hicho cha kuvunjiwa heshima Kitabu chao Kikakatifu, huku ikiwapa himaya na ulinzi raia wa Uholanzi waliotekeleza uafriti huo dhidi ya Qur'ani Tukufu.

Wakati huohuo, askari polisi nchini Sweden jana Ijumaa walimtia mbaroni mwanamke mmoja mwanaharakati, kwa kujaribu kuzuia kukaririwa kitendo cha kuchomwa moto Qur'ani Tukufu mjini Stockholm. 

Polisi ya Sweden yamshambulia mwanaharakati 

Video iliyosambaa mitandaoni inaonesha mwanamke huyo akimnyunyizia poda kafiri Salwan Momika, mkimbizi wa Iraq anayeishi nchini Sweden kwa kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu mjini Stockholm chini ya himaya ya polisi ya nchi hiyo ya Ulaya.

Hivi karibuni, wanachama wa kundi la wabaguzi wa rangi linalojiita Wazalendo wa Denmark walichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu mbele ya ubalozi wa Uturuki. Wanachama wa kundi hilo pia walichoma moto nakala nyingine ya Qur'ani mbele ya ubalozi wa Iraq mjini Copenhagen.

Dharau na vitendo vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Sweden na Denmark, na sasa Uholanzi vimeongezeka sana katika wiki za hivi karibuni, na vimekabiliwa na malalamiko katika nchi za Waislamu na kwenye duru za kimataifa.

Tags