Waislamu waandamana Ujerumani kupinga vitendo vya kuvujiwa heshima Qur'ani
(last modified Mon, 21 Aug 2023 13:17:36 GMT )
Aug 21, 2023 13:17 UTC

Waislamu wa Ujerumani leo wamefanya maandamano wakipinga vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Magharibi

Shirika la habari la Iranpress limeripoti kuwa, waandamanaji hao waliokusanyika mbele ya balozi za Sweden na Denmark mjini Berlin wamesisitiza kuwa, kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu ni kitendo cha kichochezi na cha kulaaniwa.

Washiriki wote katika maandamano hayo walikuwa wamebeba nakala ya Qur'ani Tukufu kama ishara ya kuheshimu kitabu hicho kitakatifu.

Hivi karibuni, wanachama wa kundi la wabaguzi wa rangi linalojiita Wazalendo wa Denmark walichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu mbele ya ubalozi wa Uturuki. Wanachama wa kundi hilo pia walichoma moto nakala nyingine ya Qur'ani mbele ya ubalozi wa Iraq mjini Copenhagen.

Dharau na vitendo vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Sweden na Denmark, na sasa Uholanzi vimeongezeka sana katika wiki za hivi karibuni, na vimekabiliwa na malalamiko katika nchi za Waislamu na kwenye duru za kimataifa.

Waislamu wa matabaka yote hasa vijana katika mitandao ya kijamii wamelaani vikali wimbi hilo la kuvunjia heshima matukufu ya kidini katika nchi za Magharibi, na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua kali dhidi ya nchi hizo ikiwa ni pamoja na kususua bidhaa za nchi hizo.