Onyo kuhusu utumiwaji wa mabomu ya vishada katika vita vya Ukraine
Utumiaji wa mabomu ya vishada katika vita vya Ukrainia na matokeo yake hatari yamewakasirisha watetezi wengi wa haki za binadamu na hata taasisi za kimataifa.
Kadiri lwamba Izumi Nakamitsu, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ameonya kuhusu hatua ya nchi za Magharibi ya kuipa Ukraine silaha hizo na kutaka matumizi yake yasimamishwe mara moja. Amesema silaha hizo ni hatari kwa maisha ya mwanadamu na zinapaswa kufutwa kabisa katika historia.
Akiashiria kwamba matumizi ya silaha katika mzozo wowote ule wa kivita huzua wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la machafuko na mivutano ya pande mbili au pande kadhaa, amesema: 'Sisi tuna wasi wasi mkubwa kuhusiana na ripoti za Ukraine kupewa silaha zilizo na urani iliyohafifishwa.'
Mabomu ya vishada ya Marekani yametumwa Ukraine katika miezi kadhaa iliyopita ambapo silaha hizo zimekuwa zikitumika kwa wingi katika vita vyake na Russia. Hii ni katika hali ambayo maafa na hasara inayosababishwa na mabomu hayo ni ya muda mrefu na hivyo kuibua wasiwasi mkubwa katika jamii.
Mark Hiznai, mkurugenzi msaidizi anayeshughulikia masuala ya silaha katika kundi la Human Rights Watch, anasema: Sehemu ya sheria za kimataifa kuhusu suala hili inahusiana na mashambulizi ya kiholela yanayowalenga raia wa kawaida.
Zaidi ya nchi 120 zimejiunga na Mkataba wa Kupiga Marufuku Matumizi ya Mabomu ya Vishada na zimekubali kuacha kutumia, kuzalisha, kuhamisha au kuhifadhi silaha hizo. Pia zimeahidi kusafisha maeneo yaliyosambazwa silaha hizo baada ya kumalizika vita. Lakini Marekani, Russia na Ukraine hazijatia saini mkataba huo na sasa Marekani imezidisha vita vya Ukraine kwa kuipa nchi hiyo silaha hizo hatari.
Mabomu ya vishada kwa kawaida huachilia idadi kubwa ya mabomu madogo madogo ambayo yanaweza kusambazwa kiholela katika eneo kubwa. Mabomu hayo huua watu wengi na yale ambayo hayakulipuka husalia ardhini kwa miongo kadhaa baada ya kumalizika vita na hivyo kuwa tishio kubwa kwa usalama wa raia wa kawaida.
Kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa, raia wa kawaida ndio huwa wahanga wakuu wa mabomu ya vishada, ambapo wanachangia asilimia 95 ya wahanga wa mabomu hayo. Aidha, asilimia 71 ya watu waliopoteza maisha kutokana na milipuko ya mabomu hayo mwaka jana walikuwa ni watoto.
Kwa kweli, mabomu ya vishada hulenga vizazi vya baadaye ambapo yale ambayo hayajalipuka hubakia ardhini kwa miaka mingi na hivyo kuhatarisha maisha ya watu wasio na hatia. Lakini pamoja na hayo majeshi ya Marekai bado yanatumia silaha hizo zilizopigwa marufuku kimataifa.
Kwa mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch, Marekani awali iliyachukulia mabomu ya vishada kuwa sehemu muhimu ya silaha zake wakati wa uvamizi wake nchini Afghanistan mwaka 2001. Kundi hilo la haki za binadamu lilikadiria kuwa muungano wa kijeshi ulioongozwa na Marekani dhidi ya nchi hiyo ya Kiislamu ulidondosha nchini humo zaidi ya mabomu 1,500 ya vishada katika miaka mitatu ya kwanza ya vita. Idara ya Ulinzi ya Marekani ilitakiwa kuacha kutumia mabomu yoyote ya vishada kufikia 2019, lakini utawala wa Donald Trump ukaondoa marufuku hiyo na kuwaruhusu makamanda wa nchi hiyo kuidhinisha matumizi yake.
Sasa, Rais Joe Biden wa Marekani, amepanua vita vya Ukraine kwa kuitumia nchi hiyo silaha hizo hatari huku akiwa na matumaini kuwa itapata ushindi wa mwisho katika vita hivyo. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya theluthi moja ya ardhi ya Ukraine imechafuliwa na mabomu hayo ya vishada. Bado haijulikani ni kwa nini Ukraine imechukua uamuzi wa kutumia mabomu ya vishada ambayo athari zake hubakia kwa uchache miaka 50, na ni kwa nini iko tayari kulipa gharama kubwa kama hiyo. Pamoja na hayo jambo lisilo na shaka ni kuwa Ukraine pia imechukua uamuzi usio wa kimaadili wala wa kibinadamu dhidi ya watu wake yenyewe.
Makundi ya haki za binadamu yanaelezea mabomu ya vishada kama "chukizo" na hata uhalifu wa kivita. Huku yakilaani kitendo cha Marekani cha kutuma mabomu ya vishada nchini Ukraine, yanakitaja kitendo hicho kuwa kosa la kuogofya sana.
Licha ya maonyo yote hayo, lakini bado mabomu ya vishada yanaendelea kutumika katika vita vya Ukrainia, mabomu ambayo yataendelea kuua watu hata baada ya vita kumalizika, kama tunavyoona mabomu ya kutegwa ardhini yakifanya katika maeneo ya vita vilivyomalizika miaka mingi nyuma.