Kuendelea hitilafu katika Umoja wa Ulaya kuhusu wahamiaji
(last modified Sun, 08 Oct 2023 02:27:24 GMT )
Oct 08, 2023 02:27 UTC
  • Kuendelea hitilafu katika Umoja wa Ulaya kuhusu wahamiaji

Hitilafu kuhusu kadhia ya wahamiaji miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya zingali zinaendelea licha ya makubaliano ya hivi karibuni kuhusu suala hilo.

Suala hilo liliangaziwa katika mkutano wa wakuu wa Umoja wa Ulaya katika mji wa Granada huko Uhispania juzi Ijumaa, ambapo mgogoro wa wahamiaji ulikuwa ajenda kuu ya mkutano huo. Suala la sera za uhamiaji za Umoja wa Ulaya na namna ya kukubaliana na wahajiri haramu au wale wanaotafuta hifadhi ilikuwa kadhia kuu iliyogubika mazungumzo ya wakuu wa Umoja wa Ulaya huko Uhispania.  

Kwa sasa, Umoja wa Ulaya na baadhi ya nchi zinazounga mkono ubunifu wa Brussels wa kuwasambaza wahamiaji katika nchi wanachama wa umoja huo, na nchi kama Hungary au Poland ambazo serikali zao za mrengo wa kulia zenye misimamo mikali zinaliona wimbi la wahamiajii haramu na raia wanaotafuta hifadhi kuwa tishio zimegawanyika. Katika hali ambayo nchi mbili hizi zinapinga makubaliano ya Umoja wa Ulaya ya kuleta mageuzi kwa ajili ya kuwafuatilia na kuwashughulikia wahamiaji haramu pale umoja huo utakapokuwa unakabiliana na wimbi kubwa la wahajiri, umoja huo unataraji kuwa makubaliano hayo yatabadilishwa na kuwa sheria kabla ya kufanyika duru ijayo ya uchaguzi wa wabunge wa umoja huo. Taasisi zisizo za kiserikali zinaamini kuwa marekebisho hayo mapya yataweza kuzidisha hatari ya wanaotafuta hifadhi kurejeshwa katika nchi zao za asili. 

Wahajiri wa Kiafrika kuelekea Ulaya 

Mabalozi wa nchi za Umoja wa Ulaya Jumatano iliyopita walifikia makubaliano ili kurekebisha  sera za uhamiaji ndani ya umoja huo. Mazungumzo yanatazamiwa kuendelea kuhusu makubaliano hayo yaliyofikiwa na wabunge wa Bunge la Ulaya. Miongoni mwa vifungu vya mpango huo wa marekebisho ya sera za uhamiaji za Umoja wa Ulaya tunaweza kutaja kurefushwa muda wa kuwashikilia raia wanaotafuta hifadhi nje ya mipaka ya Umoja wa Ulaya ikiwa watakabiliwa na mgogoro sawa na ile iliyoshuhudiwa mwaka 2015 hadi 2016. Habari za kufikia makubalianoku husu mpango huo tajwa zimeangazwa na Uhispania ambayo ni mwenyekiti wa kiduru wa  Baraza la Umoja wa Ulaya. Hii ni katika hali ambayo kwa miezi kadhaa sasa Ujerumani inapinga mpango huo wa marekebisho ya sera za uhamiaji wa Umoja wa Ulaya kwa sababu za kibinadamu. Hatimaye mawaziri wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya waliweza kuiridhisha Berlin katika mkutano wao wa Septemba mwaka huu. Hata hivyo Italia katika wiki kadhaa za karibuni imekuwa ikipinga majukumu yaliyopatiwa mashirika yasiyo ya kiserikali ya kuwaokoa wanaotafuta hifadhi katika bahari ya Mediterania. Rome pia imekosoa sera za uhamiaji za Ujerumani ambayo inayafadhili kifedha mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali yanayowahudumia wahajiri. Hatimaye Ujerumani na Italia Jumatano iliyopita zilifikia mapatano kuhusu mpango wa pamoja kuhusu wakimbizi na wanaotafuta hifadhi na hii ni katika  hali ambayo nchi za Ulaya ya Mashariki khususan Poland na Hungary kimsingi zinapinga kuwapokea wakimbizi. Nchi hizi mbili ni wapinzani wakuu wa kufanyiwa marakebisho sera za uhamiaji na zimepiga kura dhidi ya mpango huo. 

Josep Borrell Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya ametahadharisha kuwa umoja huo umegawanyika pakubwa kuhusu zera za uhamiaji na kuwa suala hilo linaweza kupelekea kuvunjika umoja huo. 

Borrell amesisitiza kuwa kuna ulazima kwa nchi  zote wananchama wa Umoja wa Ulaya  kutekeleza sera za pamoja za uhamiaji na kwamba wanachama wa umoja huo hadi sasa bado hawajaafikiana kuhusu suala la uhamiaji. Ameongeza kuwa Licha ya kuasisiwa mpaka wa nje wa pamoja, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zingali zinahitilafiana kimitazamo kuhusu namna ya kusimamia ipasavyo masuala ya uhamiaji na wahajiri.   

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa EU 

Kadhia ya wahajiri imekuwa changamoto kubwa kwa baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kwa kuzingatia kuwa nchi hizo zinatakiwa kutekeleza kila mara maamuzi ya Brussels. Nchi hizo zinakabiliwa na tatizo la mgongano kati ya mamlaka ya kujitawala na maslahi ya kitaifa kwa upande mmoja,na utekelezaji wa maamuzi na sheria za Umoja wa Ulaya kwa upande wa pili. Borell amesema, hitilafu hizo zinasababishwa na hitilafu kubwa za kiutamaduni na kisiasa zilizopo baina ya nchi wanachama wa umoja huo. Kupanuka kwa mgogoro wa wahajiri pamoja na migogoro mingine ya kiuchumi na kisiasa kumeupelekea Umoja wa Ulaya kukumbwa na changamoto kubwa katika miaka ya karibuni na hivyo kuibua hitilafu kati ya wakuu wa nchi za Ulaya. Upuuzaji na kukaa kimya nchi za Magharibi kumezidisha kila uchao matatizo ya kibinadamu na kijamii ya wakimbizi na wahamiaji haramu kutoka Afrika na katika nchi za Asia Magharibi; na hivyo kuwatumbukiza wahajiri katika njaa na umaskini mkubwa katika nchi za Ulaya. Kutumika kisiasa mgogoro wahajiri na nara za kuvutia uungaji mkono wa umma hasa kutoka kwa harakati na vyama vya mrengo wa kulia vyenye misimamo mikali kwa ajili ya kuingia madarakani kumeibua hofu kwa raia na kueneza hisia za kupinga wahamiaji katika jamii za Ulaya. 

 

Tags