Putin: Israel imepora ardhi halali ya Wapalestina kwa kutumia jeshi
Rais Vladimir Putin wa Russia amesema utawala haramu wa Israel umenyakua sehemu kubwa ya ardhi ya halali ya Wapalestina kwa kutumia vikosi vya jeshi la utawala huo wa Kizayuni.
Rais Putin alisema hayo jana Jumatano akihutubia Mkutano wa Wiki ya Nishati ya Russia mjini Moscow na kuongeza kuwa, "Matatizo ya Palestina yapo katika mioyo ya kila anayejitambua kuwa Muislamu, na wanaamini kuwa chimbuko lake ni dhulma iliyofikia daraja isiyofikirika."
Rais wa Russia amebainisha kuwa, kadhia ya Palestina ipo katika moyo wa kila mtu katika eneo hili. Amesema Wapalestina wameshuhudia kila aina ya jinai na dhulma si muda huu tu, bali katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita.
Amesisitiza kuwa, utatuzi wa mgogoro wa Palestina ni kutekelezwa maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kutangazwa nchi huru ya Palestina.
Rais Putin ameongeza kuwa, "Ingawaje ardhi za Palestina daima zinatambulika kuwa milki halali ya Wapalestina, lakini sehemu ya ardhi hiyo imeporwa na Israel katika nyakati tofauti na kwa kutumia mbinu tofauti; lakini mbinu kuu ni utumiaji wa nguvu za kijeshi."
Haya yanajiri huku wanamuqawama wa Palestina wakiendelea na mapambano yao ya kishujaa ya kukabiliana na wanajeshi makatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika vitongoji kadhaa vya karibu na Ukanda wa Gaza.
Zaidi ya Wazayuni 1,200 wameshaangamizwa na zaidi ya 2000 wengine wamejeruhiwa, na idadi isiyojulikana wako mikononi mwa wanamapambano wa Palestina tangu ilipoanza Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa Jumamosi iliyopita.