Kushtadi mvutano baina ya Russia na utawala wa Kizayuni wa Israel
Mvutano baina ya Russia na utawala ghasibu wa Israel umeshadidi baada ya ziara ya wawakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) mjini Moscow.
Kuhusiana na suala hilo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya utawala wa Kizayuni wa Israel imemuita Anatoly Viktorov, balozi wa Russia katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel na kulalamikia safari ya ujumbe wa Hamas kwenda Moscow.
Kulingana na ripoti zilizochapishwa, wajumbe wa Hamas, wakiongozwa na Musa Abu Marzouq, mjumbe mwandamizi wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya HAMAS, walikutana na kufanya mazungumzo na maafisa kadhaa wa kisiasa wa Russia. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia imetangaza katika muktadha huu kwamba wakati wa mkutano na ujumbe wa Hamas, walijadili suala la kuachiliwa huru kwa mateka na kuhamishwa kwa raia wa Russia kutoka Ukanda wa Gaza.
Harakati ya Hamas nayo ilisifu msimamo wa Rais Vladmir Putin wa Russia kuhusiana na mzozo kati ya Wapalestina na Israel na juhudi za kidiplomasia za Moscow za kusitisha vita huko Gaza. Balozi Simona Halperin, Naibu Mkurugenzi wa kitengo cha Eurasia katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Israel amesema: Tel Aviv inauchukulia kwa uzito mkubwa msimamo wa Moscow wa kutoilaani waziwazi HAMAS.
Uhusiano kati ya utawala wa Kizayuni na Russia umekuwa wa mvutano katika miaka iliyopita, ukiathiriwa na hali ya kisiasa na matukio ya eneo hili. Mivutano hii imekumbana na hali ya panda na shuka baada ya mgogoro wa Syria na kuingia kwa Moscow katika mgogoro huu na sisitizo lake la haja ya kuhifadhiwa ardhi na mamlaka ya ardhi ya Russia. Lakini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kutokana na vita vya Ukraine, mivutano kati ya Russia na utawala wa Kizayuni imeongezeka zaidi. Ushirikiano wa utawala wa Kizayuni na Ukraine pamoja na nchi za Magharibi hususan kufuata siasa za Washington kuhusu Kiev, umeongeza mvutano kati ya Moscow na Tel Aviv.
Kutumwa silaha za kijeshi na Israel nchini Ukraine na uungaji mkono wa sera za Marekani, ikiwa ni pamoja na uungaji mkono wa sera za vikwazo vya madola ya Magharibi dhidi ya Russia, kuliifanya Moscow kuchukua hatua dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Homa ya mzozo baina ya Russia na Israel ilipanda zaidi kiasi cha kufikia Moscow kuionya Tel Aviv kwa hatua zake za kuipatia silaha Ukraine na kulisaidia taifa hilo katika vita dhidi ya Russia.
Mivutano hii imeshtadi zaidi katika miezi ya hivi karibuni kutokana na kushadidi kwa vita nchini Ukraine na misimamo ya Israel dhidi ya Russia. Kiasi kwamba muda si mrefu uliopita, baada ya mkutano kati ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Moscow iliufuta utawala wa Kizayuni kutoka katika soko la hisa la Russia.
Katika wiki za hivi karibuni, sambamba na kuongezeka kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina, serikali ya Moscow daima imekuwa ikitoa mwito wa kukomeshwa mashambulizi ya Israel na kusitishwa mapigano. Kutokana na mashambulizi ya mfululizo ya utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya watu wa Gaza, maelfu ya raia wameuawa na kujeruhiwa katika kipindi cha wiki chache zilizopita. Wakati huo huo, Marekani na washirika wake wamekusanya rasilimali zao zote kusaidia utawala wa Kizayuni.
Wakati jumuiya ya kimataifa ikilaani jinai za Israel na kuwasilishwa mipango mbalimbali ya kuhitimisha mgogoro wa sasa, viongozi wa utawala wa Kizayuni wamesema mara kwa mara katika siku chache zilizopita kwamba, hawako tayari kukubali usuluhishi ili kukomesha mashambulizi dhidi ya wananchi wa Gaza. Suala hili limevuta hisia za maafisa wakuu wa Russia. Katika muktadha huo Rais wa Russia Vladmir Putin amesema: Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kufikiria kuhusu raia wanaoteseka kutokana na mashambulizi hayo, na kwamba, Russia inatangaza utayari wake wa kusaidia juhudi za kuhitimisha mapigano baina ya wanamapambano wa HAMAS na jeshi la Israel.
Licha ya tangazo la Russia na juhudi zake za kuwa mpatanishi, lakini mashambulizi ya mabomu ya Israel dhidi ya Gaza yanaendelea. Filihali safari ya ujumbe wa Hamas mjini Moscow imelipua hasira za viongozi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Russia.
Amir Weitmann, mmoja wa wajumbe wa ngazi za juu wa chama cha LIKUD na mshauri wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema kuhusiana na jambo hilo: Russia inamuunga mkono adui wa Israel. Sisi tutaibuka na ushindi katika vita hivi na hatuwezi kusahau kwamba, nyinyi mnafanya nini, na sisi tunakuja ili tupate uhakika kwamba, Ukraine inapata ushindi ili tupate uhakika kwamba, mtalipa gharama ya kile mlichokifanya.
Kwa kutilia maanani misimamo ya ukosoaji ya Russia dhidi ya utawala wa Kizayuni na misimamo ya chuki ya Tel Aviv dhidi ya hatua hiyo ya Moscow hususan mkutano wa viongozi wa Russia na maafisa wakuu wa Hamas, inatarajiwa mivutano ya kisiasa kati ya pande hizo mbili itashadidi zaidi katika siku zijazo.