Kiongozi wa upinzani: Zelensky atakuwa rais wa mwisho wa Ukraine
Kiongozi wa zamani wa upinzani wa Ukraine amekosoa vikali mienendo ya Rais wa nchi hiyo, Volodymyr Zelensky na kusema kuwa, yumkini mwanasiasa huyo atakakuwa rais wa mwisho wa Ukraine.
Viktor Medvedchuk alisema hayo jana katika makala aliyoiandika ambapo amesisitiza kuwa, Zelensky anafaa kujilaumu mwenyewe kwa matatizo yanayomsumbua sasa na yatakayomsibu hapo baadaye.
Medvedchuk amemtaja Zelensky kama bingwa wa usaliti, mtu asiye na huruma na mwanasiasa ambaye hulka yake ya 'kumpiga jambia kwa nyuma' kila anayetangamana naye imelitumbukiza taifa la Ukraine kwenye migogoro.
Kiongozi huyo wa zamani wa upinzani wa Ukraine ameeleza kwenye makala hiyo kuwa: Zelensky baada ya kuchaguliwa rais kwa kutumia suala la amani na Russia na maridhiano na eneo la Donbass, aliwaachia madaraka ya nchi wanasiasa wenye misimamo ya kuchupa mipaka ya utaifa.
Medvedchuk ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni Russia amesema Rais Zelensky alilisaliti taifa na kuwasaliti wapiga kura waliomchagua, kwa kwenda kinyume na ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais.
Kwa mujibu wa Medvedchuk, Marekani ilimtumia Zelensky kama chombo cha kuyashinikiza mataifa ya Ulaya yatoe muhanga chumi zao kwa maslahi ya Ukraine.
"Zelensky si tu alisaliti maslahi ya Ukraine, bali pia maslahi ya Ulaya," ameeleza mwanasiasa huyo wa upinzani wa Ukraine anayeishi nchini Russia.
Amesema: Zelensky hivi sasa amebaki peke yake baada ya kuunda udikteta wa Kinazi na kijeshi nchini Ukraine, na hii ndiyo sababu atakuwa rais wa mwisho wa taifa la Ukraine.