Dec 01, 2023 02:29 UTC
  • Washington Post: Chama tawala India kinatumia vita vya Israel dhidi ya Gaza kuwadhihirisha Waislamu kuwa ni mashetani

Gazeti la Washington Post la Marekani limetahadharisha kuhusu mienendo ya chama tawala nchini India na jinsi kinavyotumia vibaya vita vya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na kuwadhihirisha Waislamu kuwa ni 'mashetani'.

Washington Post limeashiria ujumbe wa chama tawala nchini India BJP katika mtandao wa kijamii wa X uliosema kuwa Israel inakabiliana na kilekile iliyochabiliana nacho India baina ya mwaka 2004 na 2014.

Makala ya Washington Post linasema katika makala ya mwandishi Rana Ayoub, ambamo alieleza kuwa dhamira ya ujumbe huo ilikuwa ni kueneza madai ya eti "ugaidi wa Kiislamu" katika nchi ambayo serikali yake inawatambua Waislamu kuwa ni mashetani.

Baada ya ujumbe huo wa chama tawala cha BJP, vituo vinavyoiunga mkono serikali vilidai kwamba India na Israel zinakabiliana na adui mmoja, yaani Uislamu.

Mwandishi wa makala ya gazeti la Washington Post amedokeza kwamba mizizi ya fikra hii inarudi kwenye fikra potovu kwamba Wahindu ndio wanadamu bora zaidi ya wengine, na kwamba wazalendo wa Kihindu walikuwa wakimtukuza Kansela wa zamani wa Ujerumani, Adolf Hitler, kabla ya uhuru, na kuliona "suluhisho la mwisho" lililowasilishwa na Wanazi kutatua tatizo la Wayahudi barani Ulaya kuwa ni “somo zuri la kujifunza na kutumiwa na Wahindu dhidi ya Waislamu.”

Mwandishi huyo amesema kuwa sehemu ya mitandao ya kijamii ya India ilijawa na furaha wakati Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant aliposema: "Tunapigana na wanyama wenye sura za binadamu," kwa sababu, harakati ya Hamas katika mtazamo wa Wahundu wa mrengo wa kulia inawakilisha sio Wapalestina pekee bali Waislamu wote.

Tags