Dec 02, 2023 10:24 UTC
  • Zelensky akosoa upuuzaji wa nchi za Magharibi kwa Ukraine

Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine amezikosoa nchi za Magharibi chini ya uongozi wa Marekani kwa kuisahau Ukraine na kuipunguzia misaada nchi hiyo katika vita na Russia.

Zelenskyy ameeleza wasiwasi wake kuhusu taathira za vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza katika kupunguza uungaji mkono wa nchi wanachama wa Nato kwa Kyiv na kusema: Suala hili linaweza kupelekea misaada ya silaha ya Magharibi kwa Ukraine kukabiliwa na changamoto.   

Rais wa Ukraine ameitahadharisha Marekani akisema Moscow itazishambulia nchi wanachama wa Nato iwapo hazitaisaidia Ukraine; na kwamba wakati huo ni watoto wao ndio watalazimika kupigana vita na Warussia. 

Indhari na ukosoaji wa Rais wa Ukraine anayeungwa mkono na Magharibi kuhusu kupunguzwa pakubwa misaada ya kijeshi na silaha kwa Kyiv katika vita kati yake na Russia unaonyesha mabadiliko ya polepole yanayotekelezwa na kambi ya Magharibi inayoongozwa na Marekani kuhusu Ukraine kuelekea upande wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) baada ya kutekelezwa oparesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa na kuanza vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza. Jambo hili limewatia wasiwasi sana viongozi wa ngazi ya juu wa Ukraine. Serikali ya Biden licha ya nara zake inazotoa sasa kuhusu ulazima wa kuendelea kuiunga mkono kwa zana za kijeshi na kwa silaha Ukraine imejikita na kuzingatia pakubwa katika kuidhaminia Tel Aviv mahitaji yake ya kijeshi, na kuhusiana na hilo, katika hatua yake ya karibuni ya kuendeleza mauaji ya watu wa Gaza yanayofaywa na utawala wa Kizayuni, imetuma mabomu 100  kwa utawala wa Kizayuni ambayo kazi yale maalumu ni kubomoa minara na nyumba zilizojengwa kwa saruji. Bila shaka, Joe Biden ametuma kifurushi cha dola bilioni 106 kwa Kongresi ambacho kinajumuisha msaada wa dola bilioni 14.3 kwa ajili ya Israeli na msaada wa dola bilioni 61.4 kwa Ukraine. Pamoja na hayo, Warepublican katika Kongresi ya Marekani ambao mara kadhaa wamekosoa misaada mikubwa ya makumi ya mabilioni ya dola ya Marekani kwa Ukraine wamepasisha mpango wa msaada huru wa dola bilioni 14.3 kwa utawala wa Kizayuni hatua inayoonyesha kuwa wanataka kuendeleza misaada ya kijeshi ya Marekani kwa Ukraine kama ilivyokuwa huko nyuma. Ni wazi kuwa Warepublican katika Bunge la Wawakilishi la Marekani wamepasisha mpango huo uliopendekezwa kwa ajili ya utawala wa Kizayuni kwa kutenganisha na bajeti ya misaada kwa Taiwan na Ukraine, na misaada ya kibinadamu ili misaada hiyo iwasilishwe haraka kwa utawala wa Kizayuni. Huko nyuma Biden alitishia kuwa ataupiga veto mpango wowote wa misaada kwa Tel Aviv bila ya kuipatia misaada Kyiv hata kama mpango huo ungeidhinishwa na Seneti.  

Rais Joe Biden wa Marekani 

Katika upande mwingine, kukiri Rais wa Ukraine kuhusu nafasi muhimu ya misaada ya nchi za Magharibi na hasa Marekani katika kuendelea vita kati yake na Russia na kulazimika Kyiv kurudi nyuma katika medani za vita iwapo itakatiwa misaada kunaonyesha namna nchi za Magharibi zilizokuwa na mchango mkuu na zilivyoisaidia pakubwa Ukraine katika kuendeleza vita vya umwagaji damu huko Ukraine, ambavyo vimeingia katika mwezi wake wa 22. Marekani ikiwa kinara na kiongozi  wa kambi ya Magharibi na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) imefanya juhudi kubwa za kupanua wigo wa vita vya Ukraine lengo likiwa ni kuidhoofisha Russia kadiri inavyowezekana na kuwasababishia Warussia maafa ya kiroho na silaha. Viongozi wa ngazi ya juu wa Marekani na Nato wanaamini kuwa ushindi wa Russia katika vita kati yake na Ukraine pamoja na Nato vina maana ya kutokuwa na itibari muungano huo; vita ambavyo vitapelekea kuongezeka pakubwa ushawishi na nguvu ya kieneo na kimataifa ya Russia huku mlingano wa kiusalama, kijeshi na kisiasa barani Ulaya ukiwa kwa madhara ya Magharibi. Kwa hiyo, licha ya mashinikizo ya wazi kwa Kyiv ili ikubali kusitisha mapigano na kutia saini makubaliano ya amani na Russia lakini hakuna shaka kuwa Wamagharibi wanataka kuendeleza vita huko Ukraine. 

Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia anasema kuhusiana na suala hili kwamba:" Moscow haioni ishara yoyote kutoka Kyiv na nchi za Magharibi kuhusu kuwa tayari pande hizo kutatua kwa njia za kisiasa mgogoro wa Ukraine. 

Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia 

Viongozi wa ngazi ya juu wa Ukraine akiwemo Zelenskyy mwenyewe hivi karibuni walikiri kuwa mashambulizi ya vikosi vya Ukraine katika msimu wa joto yamepelekea kupungua hamu ya nchi za Magharibi ya kutuma misaada kwa nchi hiyo. Katika uwanja huo, Kyiv imetambua kuwa misaada ya silaha ya Washington inayotumwa kwake wakati huu haiwezi kurejesha ardhi ilizopoteza. Pamoja na hayo yote, Rais wa Ukraine ametilia mkazo azma ya Kyiv kuendeleza vita na Russia. Zelenskyy amesema: "Hatuna uwezo wa kufikia natija nzuri lakini hili halipelekei kujiondoa vitani. Sisitizo la viongozi wa ngazi ya juu wa Ukraine kwa ajili ya kuendeleza vita vya umwagaji damu huko Ukraine kwa kuzingatia maafa na hasara kubwa ilizopata nchi hiyo katia vita na Russia ni la kushangaza. Sergei Shoigu Waziri wa Ulinzi wa Russia jana alitangaza kuwa jeshi la Ukraine limefeli katika mashambulizi yake dhidi ya vikosi vya Russia yaliyotekelezwa kuanzia mwezi Juni dhidi ya ngome za jeshi la Russia. Katika makabiliano hayo, Ukraine ilipoteza wanajeshi wake 125,000 na aina mbalimbali za silaha 16,000.

 

Tags