Dec 05, 2023 02:38 UTC
  • Marekani yakiri kushindwa suluhisho la kijeshi kwa mgogoro wa Ukraine

Jenerali Charles Brown Jr, Mkuu wa Kamandi ya Pamoja ya Jeshi la Marekani, huku akibainisha kwamba vita daima humalizika kwa makubaliano ya kidiplomasia, amesisitiza kuwa mzozo wa Ukraine hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi.

Akijibu swali iwapo vita vya Ukraine vitamalizika kwa Ukraine kupata kila inachotaka kutoka kwa Russia, Brown amesema: Hakuna mzozo wa kijeshi unaotatuliwa kikamilifu kwa njia za kijeshi, bali hatimaye njia ya kidiplomasia itatumika kumaliza mzozo huo.  Akieleza kuwa hawezi kutabiri matukio ya siku zijazo, amesema: 'Washington haiweza kumaliza vita kwa kuendelea kuiunga mkono Ukraine na kuitumia silaha na zana inazohitajia.'

Msimamo wa Washington kuhusu vita vya Ukraine, uliotolewa na mkuu huyo wa majeshi ya Marekani, unaonyesha kuwa nchi hiyo, ikiwa mwitifaki mkubwa na muhimu  wa Ukraine katika vita na Russia, imefikia natija kuwa vita vya Ukraine haviwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi na njia ya kidiplomasia ndio suluhisho pekee la mgogoro huo. Suala hili lina umuhimu mkubwa hasa kwa kuzingatia kushindwa kijeshi Ukraine katika mikoa yake ya mashariki na kusini mashariki ambapo imepata hasara kubwa na kuharibiwa vifaa na zana zake nyingi za kijeshi. Alexey Arstevich, makamu wa rais wa zamani wa Ukraine, amesema kuwa Ukraine imepoteza wanajeshi 300,000 katika vita na Russia.

Licha ya matumaini makubwa ya NATO na Marekani ya kushindwa majeshi ya Russia na kuondoka katika ardhi ya Ukraine, lakini kiutendaji, Warussia kwa kutumia mbinu na vifaa vinavyofaa wameweza kukabiliana na mashambulizi hayo na hata kuteka baadhi ya ardhi mpya za Ukraine. Hivi sasa Volodymyr Zelensky, rais ambaye ana mielekeo ya Kimagharibi wa Ukraine amekubaliana na ukweli kwamba kutokana na vita vya Gaza, nchi za Magharibi hususan Marekani zimeshughulishwa na mgogoro wa utawala wa Kizayuni na makundi ya wanamapambano wa Kipalestina. Licha ya ukosoaji na malalamiko ya Zelensky, ama kidhahiri matakwa yake ya kuendelezwa vita na hata kuongezwa misaada ya kijeshi na silaha hayajapewa muhimu na nchi Magharibi. Licha ya ukweli kwamba Jenerali Brown ameahidi katika mazungumzo yake kuendelea kutuma silaha na zana zinazohitajiwa na Ukraine, lakini kutokana na kuongezeka upinzani ndani ya Marekani, hasa kutoka kwa wabunge wa chama cha Republican, kuendelea kutolewa misaada ya Washington kwa Kyiv kama ilivyokuwa imezoeleka ni jambo litakalokuwa gumu kutekelezeka.

Wanajeshi wa Ukraine

Jambo muhimu ambalo wakuu wa majeshi ya Marekani pia wamelikiri ni Ukraine kutumika katika makabiliano ya Washington na Russia, hasa katika jukwaa la Ulaya. Akisisitiza juu ya umuhimu wa uungaji mkono wa Washington kwa Kyiv, Charles Brown Jr. amesema: Uungaji mkono kwa Ukraine ni kwa kuzingatia malengo ya muda mrefu ya Washington ya kuimarisha satwa yake katika kukabiliana na Moscow. Serikali ya Biden inaamini kwamba ushindi wa Moscow katika vita vya Ukraine utapelekea nchi hiyo kuendelea kukalia maeneo iliyoyateka na hivyo kuimarika ushawishi na nguvu ya Russia kieneo na kimataifa, na jambo hilo huenda likabadilisha uwiyano wa kijeshi, kiusalama na kisiasa barani Ulaya  kwa madhara ya Marekani na NATO. Kidhahiri Washington inataka vita viendelee huko Ukraine, licha ya kuishinikiza  Kyiv ikubali kusitisha mapigano na kutia saini makubaliano ya amani na Russia.

Suala jingine lenye muhimu katika jitihada za Marekani za kudumisha vita nchini Ukraine na kuendelea kukabiliana na Russia na Ulaya ni faida za kiuchumi zinazotokana na biashara ya nishati katika nchi za Ulaya kutokana na kupungua na hata kusimamishwa uagizaji wa gesi kutoka Russia na kuongezeka uagizaji wa gesi asilia kutoka Marekani. Kwa mujibu wa  Shirika la Takwimu la Ulaya (Eurostat), tangu kuanza vita vya Ukraine makampuni ya Marekani yamepandisha bei ya gesi mara mbili kwa nchi za Umoja wa Ulaya ambayo ni karibu euro bilioni 66.7. Hata hivyo, Moscow imetangaza kuwa licha ya vikwazo baadhi ya nchi za Ulaya bado zinaendelea kununua mafuta na gesi yake kupitia upande wa tatu, lakini kwa bei ya juu. Kwa hivyo, Washington inatumai kwamba kuendelea uhusiano mpya wa gesi katika pande zote za Bahari ya Atlantiki, utazifanya nchi za Ulaya kuwa wateja wake wa kudumu wa kununua gesi asilia.

 

Tags