Pakistan na kupinga ripoti ya Marekani kuhusu ugaidi
Ikionyesha masikitiko yake juu ya ripoti ya kila mwaka ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuhusu ugaidi, Pakistan imeyaona madai ya Washington dhidi ya Islamabad kuwa ni upotoshaji wa ukweli na uhalisia wa mambo.
Zahra Mumtaz Baloch, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ameeleza masikitiko yake kwamba, jukumu la nchi hiyo katika vita dhidi ya ugaidi na kuzuia ufadhili wa magaidi lilipuuzwa. Baada ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya Afghanistan, George Bush mtoto aliyekuwa Rais wa wakati huo wa Marekani aliitangaza Pakistan kuwa ni mshirika wa Washington asiye wa NATO, lakini baada ya muda mfupi, Marekani iliishutumu Pakistan kwa kutokuwa mwaminifu katika kushirikiana na Washington katika kile kinachoitwa mapambano dhidi ya ugaidi. Kwa msingi huo sherehe ya fungate kati ya Marekani na Pakistan ikawa imefikia tamati. Baada ya hapo, ilianza kuandamwa na tuhuma nyingi kutoka kwa maafisa wa kisiasa na kijeshi wa Marekani.
Morteza Haider, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na suala hilo: "Marekani ilitarajia Pakistan itii kikamilifu maombi ya Washington hasa kutokana na kuipatia nchi hiyo misaada wa kijeshi na kifedha. Hii ni katika hali ambayo inaonekana kuwa, Pakistan inatekeleza sera zake za kigeni hususan huko Afghanistan katika fremu ya maslahi yake kitaifa jambo ambalo haliifurahishi kabisa Washington.
Viongozi wa Pakistan wanasema kuwa, Islamabad ina ufahamu na welewa kamili wa majukumu yake ikiwa nchi huru na yenye mamlaka kamili na kwamba, madai yaliyotolewa dhidi yake katika ripoti ya kila mwaka ya Marekani kuhusu ugaidi inaipinga kwani haina maana wala msingi wowote.
Hitilafu baina ya Pakistan na Marekani zilishadidi zaidi katika kipindi cha urais wa Donald Trump ambapo mwanasiasa huyu aliituhumu waziwazi Pakistan kwamba, inaunga mkono ugaidi na akakta misaada ya kifedha na kijeshi ya nchi yake kwa serikali ya Islamabad.
Inaonekana kuwa, katika kipindi cha utawala wa Rais Joe Biden siyo tu kwamba, hakujatokea mabadiliko katika uhusiano wa Washington na Islamabad, bali uhusiano huo umetumbukia nyongo zaidi. Si jambo lililo mbali kwamba, matukio ya miaka miwili na nusu iliyopita huko Afghanistan yamekuwa kikwazo cha kuboreka uhusiano wa Pakistan na Marekani. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, Marekani ilikuwa ikitaraji kuwa, Pakistan kwa kusimamia vyema matukio ya Afghanistan hususan Taliban ingesaidia kutekeleza sera za ikulu ya White House huko nchini Afghanistan.
Ahmad Mansour Khan, mweledi wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na hili kwamba: Kwa kushirikiana na Marekani, serikali ya Pakistan inataraji kuiona Washington nayo ikisaidia kudhamini maslahi ya kitaifa ya Islamabad ikiwemo kadhia ya Kashmir; lakini hatua ya Marekani ya kuichagua India ambayo ni hasimu wa Pakistan maana yake ni kuwa, Islamabad na Washington zina hitilafu za kimkakati katika masuala mbalimbali ikiwemo kadhia ya Kashmir na matukio ya Afghanistan.
Alaa kulli haal, kwa mujibu wa vingozi wa Pakistan ni kuwa, katika ripoti yake hiyo Marekani haijaashiria hata kidogo mchango wa Pakistan katika kusambaratisha mitandao ya kimataifa ya ugaidi. Hii ni katika hali ambayo, zaidi ya askari 80,000 wa vikosi vya usalama na raia wa Pakistan wameuawa katika vita dhidi ya ugaidi na Islamabad imepata hasara ya mamia ya mabilioni ya dola.
Inaonekana kwamba kumekuwa na tofauti kati ya Marekani na Pakistan kuhusu fasili, maana na kielelezo cha ugaidi. Katika hili Pakistan inaituhumu Marekani kwa kutekeleza sera za uharibifu nchini Afghanistan, kiasi kwamba, Islamabad imeelezea mara kwa mara wasiwasi wake kuhusu hali ya Afghanistan na matokeo yake ya hatari kwa mataifa mengine ya eneo.
Pakistan inasema kuwa, kuondoka kusiko kwa uwajibikaji kwa askari wa Marekani na NATO huko Afghanistan, kumepelekea kushadidi vurugu na machafuko katika nchhi hiyo. Tofauti kati ya Pakistan na Marekani zimezidi kupamba moto huku matukio ya Afghanistan nayo yakionekana kuwa nje ya udhibiti wa Islamabad, jambo ambalo linaonekana kutokubalika na Washington. Kwa muktadha huo, si jambo lililo mbali kuona Marekani ikiongeza mashinikizo yake dhidi ya Pakistan.