WHO yaonya: Sigara za kielektroniki zina athari mbaya, zidhibitiwe
https://parstoday.ir/sw/news/world-i106012-who_yaonya_sigara_za_kielektroniki_zina_athari_mbaya_zidhibitiwe
Shirika la Afya Duniani WHO limesema hatua za haraka zinapasa kuchukuliwa kudhibiti sigara za kielektroniki ili kulinda watoto pamoja na wasiovuta sigara na kupunguza madhara ya kiafya kwa watu.
(last modified 2026-02-17T17:08:55+00:00 )
Dec 15, 2023 06:54 UTC
  • WHO yaonya: Sigara za kielektroniki zina athari mbaya, zidhibitiwe

Shirika la Afya Duniani WHO limesema hatua za haraka zinapasa kuchukuliwa kudhibiti sigara za kielektroniki ili kulinda watoto pamoja na wasiovuta sigara na kupunguza madhara ya kiafya kwa watu.

WHO imeeleza kuwa, sigara za kielektroniki hazioneshi kuwa na ufanisi katika kuacha matumizi ya tumbaku badala yake na kwamba ushahidi wa kutisha umeibuka juu ya athari zake mbaya za kiafya kwa watu.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema: "watoto wanaingia na kunaswa wakiwa wachanga ili kutumia sigara za kielektroniki na wanaweza kuhusishwa na nikotini. Ninazisihi nchi kutekeleza hatua kali za kuzuia matumizi ili kulinda raia wao, hasa watoto wao na vijana".

 Dkt. Ruediger Krech, Mkurugenzi wa Kukuza Afya wa WHO amebainisha kwamba, sigara za kielektroniki zinalenga watoto kupitia mitandao ya kijamii na vishawishi vyenye takribani ladha 16,000.

Imeelezwa kuwa, sigara za kielektroniki zilizo na nikotini hulevya sana na ni hatari kwa afya. Ingawa athari za kiafya za muda mrefu hazijaeleweka kikamilifu, lakini imethibitishwa kwamba hutoa vitu vyenye sumu, ambavyo vingine vinajulikana kusababisha saratani na vingine huongeza hatari ya magonjwa ya moyo na mapafu.

Aidha, utumiaji wa sigara za kielektroniki unaweza pia kuathiri ukuaji wa ubongo na kusababisha matatizo ya kujifunza kwa vijana. Sigara hizo zinaweza kuathiri vibaya ukuaji wa kiinitete kwa wanawake wajawazito. Pia moshi unaotoka kwenye sigara za kielektroniki ni hatari kwa watu walio karibu na mvutaji.

Sigara za kielektroniki katika maeneo mengi duniani zimeruhusiwa kwenye soko la wazi na kuuzwa sana kwa vijana.../