Maandamano ya wananchi wa Uturuki ya kupinga vita
Katika muendelezo wa maandamano ya kupinga mauaji ya kimbari ya Waislamu huko Gaza, makumi ya maelfu ya wananchi wa Uturuki wamefanya maandamano makubwa mjini Istanbul kupinga jinai za utawala wa Kizayuni na mauaji ya vijana wa Kituruki kaskazini mwa Iraq katika siku ya kwanza ya mwaka huu mpya wa 2024.
Wananchi na viongozi mbalimbali wa Istanbul Jumatatu ya juzi tarehe Mosi Januari walijitokeza tena mitaani na kulalamikia mauaji ya wanajeshi 12 wa Uturuki kaskazini mwa Iraq na kuendelea mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na hatia wa Gaza.
Maandamano hayo yalifanyika kwa uratibu na mpango wa Jukwaa la Utashi wa Kitaifa katika fremu ya mashirika 308 yasiyo ya kiserikali. Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walipiga nara kama vile, Allah awarehemu mashahidi wetu. Aidha walitoa nara za kuulaani utawala ghasibu wa Israel na kutangaza himaya na uungaji mkono wao kwa wananchi madhulumu wa Palestina hususan wa Ukanda wa Gaza ambao wanapitia kipindi kigumu cha masaibu na ukatili wa Israel.
Kimya cha namna fulani cha viongozi wa serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan kwa mauuaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza kimepelekea kufanyika maandamano ya mara kwa mara nchini Uturuki katika kipindi cha takribani miezi mitatu tangu kuanza hujuma na mashambulio ya kinyama ya Israel huko Gaza.
Sambamba na maandamano ya wananchi Waislamu wa Uturuki, wachambuzi wa masuala ya kisiasa pia wanapinga siasa za kinafiki za serikali za Magharibi kuhusiana na jinai zinazoendelea Israel na daima wanafichua siasa za serikali za Magharibi. Mapitio ya ya yale yaliyoandikwa kwenye magazeti ya "Sabah", "Hurrit", "Karar", "Yeni Akit" na vituo vingi vya masuala ya utafiti wa maudhui mbalimbali vya Kituruki yanaonyesha kwamba, wachambuzi wengi wa Kituruki wanaamini kuwa, mtazamo wa sasa wa nchi za Magharibi kuhusiana na matukio ya Gaza, hauna uwiano na kaulimbiu zao za haki za binadamu na jinsi walivyolipigia upatu suala la haki za binadamu.
Ahmad Tashgatiren amesema kuhusu mtazamo wa Wamagharibi kuhusu matukio ya sasa ya Gaza:
"Mashambulio ya kinyama ya mabomu dhidi ya Gaza yanaendelea. Kila siku idadi ya vifusi inazidi kuongezeka. Kila siku mauaji ya raia wakiwa na picha za watoto wachanga mikononi mwao yanaongezeka. Lakini uungaji mkono wa Marekani na washirika wake kwa Israel bado unaendelea kuongezeka. Hatua hizo zinamaanisha kwamba viongozi wa nchi za Magharibi, kiutendaji, sio tu kwamba hawana tatizo na mauaji ya Israel huko Gaza, bali pia wana ushindani baina yao wa kumuunga mkono muuaji.
Licha ya ukosoaji wa wananchi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa wa vyombo vya habari vya Uturuki kuhusu jinai za utawala wa Kizayuni, lakini serikali ya Recep Tayyip Erdogan ingali inafuatilia masuala kama vile mazungumzo na kujaribu kutangaza usitishaji vita kati ya pande zinazozozana.
Fauka ya hayo, serikali ya Uturuki imekataa hata kumfukuza balozi wa Israel mjini Istanbul. Wakati huo huo, ukosoaji wa wanasiasa wenye mafungamano na vyama vingine vya upinzani kwa sera za serikali ya Erdogan umeongezeka zaidi, kiasi kwamba, vingozi wa vyama vya upinzani vya Uturuki wametangaza kuwa, marufuku ya Nescafe na Coca-Cola kwenye menyu (orodha ya chakula) ya Bunge la Uturuki haina maana yoyote. Kama mnasema kweli simamisheni usafirishaji wa bidhaa ya chuma kwa Israel. Ripoti zinaonyesha kuwa, Uturuki ni msafirishaji mkuu wa bidhaa ya chuma kwa utawala ghasibu wa Israel. Israel inatengeneza mabomu kwa kutuma chuma chetu.
Suala jingine muhimu lililotolewa katika nara za makumi ya maelfu ya raia wa Istanbul walioandamana hapo juzi ni suala la mauaji ya wanajeshi wa Uturuki kaskazini mwa Iraq. Watu wa Uturuki wanatarajia kila siku kuona kwamba vita vya serikali ya Erdogan na nchi jirani vinamalizika. Aidha wanasema kuwa, wanajeshi wa Uturuki wanapaswa kurejea majumbani mwao na kwa familia zao, na mauaji ya Waislamu kwa kisingizio chochote yanapaswa kufikia tamati.
Siku moja jeshi la Uturuki linawaua Wakurdi kadhaa wakiwemo wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK) kwa ndege isiyo na rubani, na siku nyingine kwa msaada wa Marekani na washirika wake, PKK inaingia na kushambulia kambi ya wanajeshi na kusababisha maafa. Hapana shaka kuwa katika hali hii, kuhitimisha mizozo hii na kufanya mazungumzo ili kupata amani ni hatua ambayo inaweza kuambatana na uungaji mkono wa wananchi Waislamu wa Uturuki.