Marekani inanunua mafuta kutoka Russia licha ya kujiwekea marufuku ya uagizaji
Marekani imeendelea kununua mafuta ya Russia licha ya kuwa mtetezi mkuu wa vikwazo dhidi ya nchi hiyo na kujiwekea marufuku tokea mwanzoni mwa mwaka 2022 ya kuagiza nishati kutoka nchini humo.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Alkhamisi ya shirika la habari la RBK likinukuu data kutoka hifadhidata ya takwimu za biashara ya nje ya Marekani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika mwezi wa Novemba pekee, Marekani iliagiza nje ya nchi karibu mapipa 10,000 ya mafuta ghafi ya Russia, yenye thamani ya $749,500.
Wakati vikwazo vya mafuta vya Washington, vilivyoanzishwa sambamba na vikwazo vikubwa vya Magharibi dhidi ya Moscow katika kukabiliana na mzozo wa Ukraine, vinakataza uagizaji wa bidhaa ghafi kutoka nchi hiyo, Marekani ingali inaruhusu kununuliwa mafuta hayo kwa kutumia kibali maalumu kutoka Ofisi ya wizara yake ya Fedha ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC).
Uagizaji wa mafuta hayo mwezi Novemba unaaminika kuwa muamala wa kwanza uliofanywa na Marekani moja kwa moja wa kununua mafuta kutoka Russia tangu ilipowekwa marufuku hiyo.

Hata hivyo, Marekani imeendelea kununua bidhaa hiyo kupitia nchi ya tatu, kulingana na ripoti ya hivi majuzi ya taasisi ya Global Witness, iliyonukuu data za ufuatiliaji wa safari za meli ya Kpler. Taasisi hiyo ya uchunguzi imegundua kuwa, katika robo tatu za kwanza za mwaka jana, Marekani iliagiza nje mapipa milioni 30 ya mafuta yaliyopatikana kupitia mitambo inayosafisha mafuta ya Russia.
Ununuzi huo ulifanywa kupitia kile wakala alichokiita "mwanya wa usafishaji mafuta," ambao unaruhusu mafuta kuingia Marekani mara tu yanaposafirishwa na kusafishwa nje ya Russia.../