Guterres asisitiza udharura wa kufanyika marekebisho katika Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i107340-guterres_asisitiza_udharura_wa_kufanyika_marekebisho_katika_umoja_wa_mataifa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza haja ya kufanyika marekebisho katika muundo wa Baraza la Usalama la shirika hilo la kimataifa.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 18, 2024 00:12 UTC
  • Antonio Guterres
    Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza haja ya kufanyika marekebisho katika muundo wa Baraza la Usalama la shirika hilo la kimataifa.

Antonio Guterres alisema jana Jumatano kwenye mkutano wa Jukwaa la Uchumi la Dunia huko Davos, Uswisi kwamba marekebisho ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ajenda mpya inayopendekezwa inaweza kusaidia kutatua na kuizuia migogoro.

Guterres ameongeza kuwa, marekebisho katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanaweza kuruhusu nchi zinazoendelea kuwa na sauti katika medani ya kimataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa taasisi zilizopo katika nyanja za kimataifa kama vile Baraza la Usalama zilianzishwa miaka 80 iliyopita na zinapaswa kuhuishwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Guterres pia ameonya kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na kusema kuwa, jamii ya kimataifa haijafanya lolote kusimamisha vita huko Gaza. "Ulimwengu unatazama tu vita huko Gaza huku raia, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wakiuawa na kujeruhiwa au kulazimishwa kuondoka majumbani mwao na kunyimwa fursa ya kupata misaada ya kibinadamu", amesisitiza Antonio Guterres.

Gaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, dunia inakabiliwa na mgogoro wa kuaminiana, hivyo kurejesha imani ndiyo kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu wa Davos.

Mkutano wa Kimataifa wa Davos nchini Uswisi hufanyika kila mwaka ukisimamiwa na Jukwaa la Uchumi Duniani  na kuhudhuriwa na maafisa wakuu wa serikali na wa sekta binafsi kutoka nchi mbalimbali.