Ujumbe wa HAMAS ya Palestina waitembelea Russia
Ujumbe wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina(HAMAS) umeitembelea Moscow, mji mkuu wa Russia.
Shirika la habari la Iran Press liliripoti habari hiyo jana Ijumaa, ambapo lilinukuu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ikithibitisha habari hizo za ujumbe wa HAMAS kuitembelea Moscow.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, maafisa wa Russia katika mazungumzo yao na ujumbe huo wa HAMAS wamelaani vikali mgogoro mkubwa wa kibinadamu unaoshuhudiwa katika Ukanda wa Gaza.
Aidha serikali ya Moscow imeiasa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) kuwaachia huru mateka wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
HAMAS kwa upande wake imesisitiza kuwa, utawala haramu wa Israel umeshindwa kufikia malengo yake yoyote baada ya kupita zaidi ya siku 100 za vita vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Viongozi wa HAMAS wamekuwa wakisisitiza kuwa, njia pekee ya kuwaachia huru wafungwa wa kivita wa Israel wanaoshikiliwa Gaza ni kuachiliwa huru mateka wote Wapalestina wanaoshikiliwa kinyume cha sheria katika vizuizi vya kuogofya vya Israel.
Hivi karibuni, HAMAS ilipongeza msimamo ulioonyeshwa na Russia na China katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hatua ya nchi hizo ya kulipigia kura ya turufu azimio lililopendekezwa na Marekani la kuuunga mkono utawala vamizi wa Kizayuni unaokalia ardhi za Wapalestina kwa mabavu.
Hadi sasa utawala haramu wa Israel umewaua Wapalestina zaidi ya 24,700 wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi wengine zaidi ya 60,000 katika hujuma zake za kinyama huko Gaza tokea Oktoba 7.